Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema umoja huo uko tayari kufuata mfano wa Marekani, wa kuondoa masharti ya haki miliki kwa chanjo za COVID-19, katika juhudi za kuhakikisha kuwa janga hilo linashughulikiwa kwa njia zinazoeleweka na zenye kuleta matokeo.
Hapo jana serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden ilitangaza kuunga mkono juhudi za kimataifa za kuondoa haki miliki za utengenezaji wa chanjo za Covid-19, hatua inayotoa matumaini kwa mataifa maskini yanayokumbwa na changamoto ya kupata chanjo hizo za kuokoa maisha.
India, ambako idadi ya vifo imefikia rekodi mpya, imekuwa ikiongoza miito ndani ya Shirika la Biashara Ulimwenguni – WTO kuziruhusu kampuni nyingi zaidi za dawa kutengeneza chanjo hiyo, hatua ambayo kampuni kubwa za dawa ziliipinga.
Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameutaja uamuzi huo wa Marekani kuwa wa “kihistoria”.