NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amekiri kuwa sasa timu yake inaweza kuonyesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na hata kutwaa ubingwa kulingana na mikakati waliyojiwekea.
Akizungumza na MTANZANIA akiwa nchini Zambia, Hall alisema kupitia mashindano hayo Azam inazidi kuimarika na kumpa uhakika wa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ambayo wataanza kushiriki mwezi Machi.
“Mashindano haya yametusaidia sana kwani nidhamu kwa wachezaji imeongezeka na kuzidi kunipa moyo wa kufanya vizuri kimataifa na katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili kukamilisha mpango wa kunyakua mataji yote makubwa,” alisema.
Alisema hawana mpango wa kutafuta mechi za kirafiki kwa maandalizi zaidi kwani mashindano wanayoshiriki yametimiza vigezo vya mahitaji yao na kupunguza gharama ambazo zingetumika kusaka mechi za kimataifa nje ya nchi.
Hall alisema kwa kutumia mashindano hayo ameweza kurekebisha makosa madogo madogo na kufanyia kazi mapungufu ambayo yamekuwa yakiwasumbua wachezaji wake mara kwa mara.
Mabingwa hao wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, wanatarajia kushuka tena dimbani Jumatano hii kuvaana na Zanaco FC ya Zambia.