26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI AAGIZA VIGOGO WA TANZANITE ONE WAACHIWE

ELIYA MBONEA Na JULIETH PETER – MIRERANI

RAIS Dk. John Magufuli  ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwaachia wawekezaji ‘wenye umuhimu’ katika migodi ya Tanzanite

ili wakakae na kamati ya kujadili madini kurekebisha mkataba uliopo uwe na faida kwa serikali na si wa unyonyaji.

Wawekezaji hao walikamatwa hivi karibuni kwa ajili ya kusaidia kutoa taarifa nyeti kuhusu madini ya Tanzanite.

Pia ameliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia SUMA JKT kuanza haraka ujenzi wa ukuta katika eneo lote la uchimbaji wa Tanzanite kutoka vitalu A mpaka D, lenye eneo la kilomita za mraba 81.99.

Eneo hilo  linatajwa kuwa na Tanzanite nyingi wakati nchini nyingine ndiyo zinaendelea kunufaika huku Serikali ikipata asilimia tano tu inayotokana na madini hayo.

Maagizo hayo  aliyatoa   jana akiwa Kata ya Naisinyai, alipozungumza na wananchi kabla ya kuzindua barabara ya kiwango cha lami kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi mji mdogo wa Mirerani, yenye urefu wa kilomita 26.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Rais Dk. Magufuli aliyeonekana kuumizwa na wizi wa   Tanzanite, alisema ameona ni vema kuanza na hatua hiyo huku akiwa na uhakika mwekezaji wa Tanzanite One na wawekezaji wengine watakaa na Serikali kutengeneza mkataba mwingine.

“Ninafahamu palikuwa na hatua kadhaa zilikuwa zimeanza kuchukuliwa kwa wawekezaji kama njia ya kupata taarifa vizuri.

“Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama…wale waliokuwa wanahusika kusaidia kutoa taarifa hizo… muwaachie wale ambao ni muhimu wakae na Kamati ya Waziri wa Sheria na Katiba, Professa Palamagamba Kabudi.

“Wapitie kwa pamoja mkataba huu waurekebishe wasaini upya ili asilimia kubwa ya fedha zibakie hapa. Fedha hizo zitakapopatikana tuanze mpango wa kuweka maji ya uhakika hapa Simanjiro.

|Nimeona tuanze na hiyo… haiwezekani wananchi wakaendelea kulia, kusikitika na wengine wakicheka kwa faida ya wanyonge.

“Nimesema hapana, ndani ya mamlaka yangu lazima tujipange vizuri. Hili suala naona linafikia mwisho, tumechezewa vya kutosha. Najua kulikuwa na watu wanafaidika, biashara ya Tanzanite haijazuiliwa bali tunaitoa kwenye magendo na kuwa biashara halali.

“Nataka Tanzanite iwe halali na si haramu, wachimbaji wadogo chimbeni, ukipata mali yako ukiwa ndani ya uzio kauze unavyotaka. “Tunataka soko la Tanzanite liwe Simanjiro si Arusha, wanaotoka Marekani na India waje wanunue hapa, akishuka na ndege hapo KIA aje kwa gari hapa anunue Tanzanite akauze anakojua,” alisema.

Huku akimsifia Mbunge wa Mererani, James ole Millya (Chadema), Rais Dk. Magufuli alisema mbunge huyo alilelewa na CCM akiwa Umoja wa Vijana (UVCCM) uliomfanya kupata ubunge hivyo hapaswi kuonekana kama adui.

“Nawashukuru kwa kumchagua Millya, ni mchapakazi amelelewa na CCM…ukimuona sura yake ni kama Chadema lakini moyo wake ni CCM kabisa,” alisema Magufuli huku akisisitiza kwamba ujenzi wa ukuta huo utakuwa na kamera na vifaa maalumu vya kubaini wizi wa madini hayo.

“Kutakuwa na mlango mmoja wa kuingilia ili kudhibiti utoroshaji. Hata ukimeza Tanzanite tumboni au kuficha kwenye viatu, itaonekana. “Ndugu zangu viongozi waliopewa mamlaka ya kusimamia rasilimali hizi kama wangezisimamia vizuri leo hii Watanzania wasingekuwa masikini.

“Kubwa linafanyika kwa sisi viongozi tunaopewa mamlaka ya kusimamia tunakuwa sehemu ya mafisadi wa kuwaumiza Watanzania maskini, viongozi tunasahau tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Tanzanite hii haitakaa miaka yote, katika uongozi wangu nimeamua kuiongoza hii vita.

“Leo nimekuja kufungua barabara, nitaifungua lakini nataka tuzungumze suala la Tanzaniate tunafanya nini?” alihoji Rais Magufuli na kuongeza:

“Sina sababu ya kumung’unya maneno, madini ya Tanzanite yanaibwa sana, ni shamba la bibi la mabibi waliokufa miaka mingi. “Watu wanachukua kuliko hata shamba la bibi. Mgodini kuna wawekezaji wameingia ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kila mtu ana asilimia 50, lakini bado mali inasombwa”.

Hivi karibuni Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One, Faisal Juma na Hussein Gonga wanaochimba Tanzanite kwa ubia na STAMICO, walikamatwa kwa mahojiano   ikiwa ni siku chache tangu Kamati ya Bunge itoe taarifa ya uchunguzi wa madini hayo iliyosomwa mbele ya Rais Dk. Magufuli.

WAWEKEZAJI

Akifafanua kuhusu wawekezaji   kuwekeza nchini, Rais Dk. Magufuli alisema Serikali inawahitaji wawekezaji wenye nia njema na si wawekezaji wanaopanga kuiibia nchi.

“Kama kutakuwa na mwekezaji anayetaka kuja nchini kutuibia basi huyo asije kabisa atakuwa amekula wa chuya kwani wakati huu hataiba bali atalia. Na hili nalisema kwa wazi, tumeamua kupambana kwa vita ya uchumi wa taifa letu.

“Nchi yetu ni tajiri, juzi tumekamata madini ya almasi yenye thamani ya fedha nyingi, kwenye madini ya dhahabu ndiyo usiombe ni uozo mtupu, ovyo,” alisema.

STAMICO

Akielezea ushiriki wa shirika hilo kusimamia madini ya Tanzanite, Rais aliagiza   baadhi ya watu walioshiriki kufanya mambo ya  ovyo waondolewe mara moja.

“Kama kuna watu waliofanya mambo ya  ovyo watolewe mara moja, ni lazima tujipange vizuri. Vyombo vya ulinzi, polisi na usalama hakikisheni  Tanzanite haivushwi  ovyo  ovyo.

“Atakayetoka na Tanzanite kwenda nje ya nchi awe halali amelipia kila kitu aende zake salama apewe na vibali.

“Tupokwenye vita kubwa ya kubadilisha hii nchi, tumechezewa mno yale ninayoyaona kule ni maajabu mengi. Nilipoingia madarakani mnafahamu tulifanya nini watumishi, wanafunzi, tumekuta hewa.

BOT

Katika mkutano huo,   kwa mara nyingine, aliiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutengeneza mkakati wa kushiriki ununuzi wa  Tanzanite kwa sababu  madini hayo si rahisi kudanganya kama inavyoweza kufanywa kwenye dhahabu.

Alishangazwa na kitendo cha mji wa Mirerani kutokuwa na gari la kubebea wagonjwa wakati kuna madini ya Tanzanite ambayo   duniani yanapatikana  katika Kata hiyo ya Naisinyai pekee.

“Hivi ni kwa nini Mungu atupe Tanzanite sisi peke yetu halafu hata gari la wagonjwa hamna? Hiyo gari nitawaletea mimi, na kuhusu suala la maji hilo pia niachieni nalifanyia kazi,” alisema Magufuli.

Naye Mbunge Millya aliyepewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo pamoja na wabunge wengine kutoka mikoa ya Manyara na Arusha, alimuomba Rais Magufuli kuhakikisha anaacha alama ya uongozi wake katika maisha ya wananchi wa Simanjiro.

“Mheshimiwa Rais Magufuli nakuomba kuja kwako kubadili maisha ya wananchi hawa waliojitokeza kukusikiliza.

“Madini ya Tanzanite yameisha, nakuomba uweke mkono wako katika ardhi ya Mirerani na Simanjiro,” alisema Millya.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Professa Makame Mbarawa alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa kiungo muhimu cha  biashara kwa wananchi wa mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles