Mokiwa: Wajumbe wa Bunge la Katiba wanapaswa kulaumiwa
NA ESTHER MBUSSI, DAR ES SALAAM
ASKOFU Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, amesema lawama zinazotolewa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kukacha Bunge Maalumu la Katiba zinapaswa kuelekezwa kwa Bunge zima.
Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu jana, alisema mwenendo mzima wa Bunge hilo umepoteza mwelekeo kwa kuacha ajenda nzima inayotakiwa kujadiliwa ambayo ni Rasimu ya Katiba Mpya na kuchukua ajenda ambayo hawakutumwa na wananchi.
Alisema wakati huu wanalaumiwa Ukawa lakini wajumbe wote wa Bunge hilo nao walaumiwe kwa kuingiza ajenda za vyama wakati wanaosimamia uendeshwaji wa shughuli za Bunge na vyombo vinavyosimamia haki wanatakiwa kusikiliza na kutazama mambo ya msingi bila kuongozwa na itikadi za vyama vyao.
Pamoja na mambo mengine, ametoa wito kwa Ukawa kurudi bungeni kujadili Rasimu ya Katiba katika Bunge hilo litakaloketi Agosti, mwaka huu.
Pia alipongeza hatua ya Kanisa Katoliki Tanzania kutoa tamko la kuwaomba Ukawa kurudi bungeni.
Alisema vita nzuri si ya kuacha viti wazi na kuwataka Ukawa warudi bungeni ili wakatoe mawazo yao humo.
“Kitendo cha kukataa kujadili pamoja ni kutoa mwanya kwa Katiba kujadiliwa na upande mmoja ambapo tutarudi kule kule kwenye Katiba ambayo inadhaniwa ni ya chama fulani.
“Lakini pia nitoe wito kama kweli kuna dhana inayodhaniwa kuna chama au vyama vinavyojaribu kumiliki mwelekeo wa upatikanaji wa Katiba wanarushiana maneno ya Kiswahili hayo tumeyasikia.
“Naviomba viache kwa sababu hatukuwatuma kwenda kutupiana risasi za maneno, tumewatuma wakatutengenezee kitu kitakachotufaa sisi na wao, sasa wasitumie nafasi hiyo kufanya wanayotaka wao,” alisema Dk. Mokiwa.
Alisema kama Ukawa wamekuwa na maumivu ya kusababishiwa na wakaamua kutorudi ni vyema wakawakumbuka wananchi wanaotazamia kitu kipya kutoka kwao kwa kuwa Taifa hili bado changa.
Alitaka kuwepo na usawa ili kufikia katika Katiba na vyama vifikirie Mtanzania anahitaji nini, aongozwe vipi kwa mujibu wa Katiba ya nchi.