32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Samia aagiza hospitali binafsi zipewe mwongozo tiba ya saratani

Aziza Masoud, Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassani, ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuandaa mwongozo maalumu kwa ajili ya hospitali binafsi zinazotibu saratani ili watoe huduma bora zitakazopunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kuzindua mashine tatu za saratani, mbili za kisasa za tiba za mionzi kwa teknolojia ya Linear Accelerators (Linac) na mashine ya kupanga (CT simulator)  zenye thamani ya Sh bilioni 9.5 zilizopo katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), alisema mwongozo huo utaelekeza pia ukaguzi maalumu wa vituo husika.

“Wizara inapaswa ihakikishe inasimamia  vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma ya saratani kwa kuwapa miongozo ya usajili pamoja na kuwakagua vitendea kazi ambavyo wanatumia ili waweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa,” alisema.

Pia alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha hakuna mgonjwa wa saratani atakayepoteza maisha katika siku za usoni.

Pia aliitaka wizara hiyo kuweka mkakati wa kuzifahamisha nchi za Malawi, Msumbiji, Sudan Kusini na Lesotho juu ya uwapo wa mashine hizo ili kuja kutibiwa nchini.

“Wizara ifanye mikakati ya kuzifahamisha nchi jirani kuhusu uwepo wa mashine hizi ili kupata rufaa za wagonjwa wengi wa nje ya nchi, hii itasaidia kuongeza mapato kwa mwaka na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini,” alisema.

Alisema wagonjwa wanaotoka nje lazima walipie matibabu, lakini hawapaswi kulipia kiwango cha kuwakomoa na kuwafukuza.

Alisema Serikali imeiwezesha taasisi hiyo vitendea kazi hivyo wanapaswa kuvitumia vizuri ili viweze kuzalisha.

Pia alisema Serikali imewekeza katika ununuzi wa mashine hizo ili wananchi wapate huduma bora zinazopatikana katika nchi za Marekani na Uingereza.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema mashine hizo za kisasa zina faida nyingi ikiwamo kuokoa fedha kwa wagonjwa waliokuwa wakienda kutibiwa nje ya nchi kwa ajili ya tiba hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles