ADDIS ABABA,Ethiopia
BINTI wa kwanza wa Rais Donald Trump, Ivanka Trump, amewasili nchini hapa kwa ajili kukuza mpango wa Serikali ya Marekani unaolenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake mahali pa kazi.
Mpango huo umelenga kuwanufaisha wanawake milioni 50 katika nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, katika ziara hiyo ya siku nne, mtoto huyo wa Rais Trump atatembelea wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya kahawa na viwanda vya nguo vinavyoendeshwa na wanawake nchini hapa kabla ya kuelekea nchini Ivory Coast.
Mpango huo wa Kimataifa wa Maendeleo ya Wanawake na Ustawi, (W-GDP) ambao ulianzishwa Februari mwaka huu una lengo la kufundisha wanawake duniani kote ili kuwasaidia kupata kazi nzuri.
Kwa mujibu wa tovuti ya mpango huo, ushiriki mdogo wa wanawake katika masoko rasmi ya ajira huzuia ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini katika nchi zinazoendelea.
Mradi huo umefadhiliwa dola milioni 50 upo ndani ya Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAid).
Tuvuti hiyo ilieleza kuwa mbali na kuwatembelea wanawake, akiwa nchini hapa, mtoto huyo wa Rais Trump, ambaye anafanya kazi kama mshauri wa baba yake atahudhuria mkutano mkuu wa Benki Kuu ya Dunia na baadae wiki hii ataelekea nchini Ivory Coast ambako atatembelea mashamba kakao pia kushiriki katika mkutano juu ya fursa za kiuchumi kwa wanawake Afrika Magharibi.