Christian Bwaya
JAMII yetu inapitia mabadiliko makubwa yanayoathiri mfumo uliozoeleka wa kimalezi.
Pamoja na hatua kubwa tuliyopiga kama jamii katika kuhakikisha kuwa akina mama wanakuwa na fursa sawa na wanaume katika soko la ajira, inavyoonekana zipo gharama zake.
Ingawa ni kweli kuwa jukumu la malezi limekuwa la wazazi wote, lakini katika jamii yetu, kwa kawaida, mama ndiye amekuwa na wajibu mkubwa zaidi. Mama huyu alikubali kubaki nyumbani kusudi aelekeze nguvu zote kwenye malezi ya watoto.
Mwanamume, tofauti na mwanamke, hakutarajiwa kutumia muda mwingi nyumbani. Ilifahamika kuwa kwake, mwanamume, jukumu lake kubwa ni kuhakikisha familia inapata kipato cha kutosha kuendesha maisha. Kwa hiyo, mwanamume alitumia muda mwingi nje ya familia akijua mama yupo nyumbani.
Katika baadhi ya makabila, ilitokea mwanamke akawa na majukumu ya kufanya kazi zaidi kuliko hata mwanamume. Ingawa mwanamke kwa kawaida hakuwa na ajira rasmi, alitarajiwa kujituma katika shughuli zinazoingiza kipato cha familia. Uwapo wa familia tandao, katika mazingira kama haya, ulimwondolea mama hofu ya nani angebaki nyumbani na mwanawe.
Wakati mama akisafiri kwenda kuuza mazao mjini, kwa mfano, nyumbani walibaki ndugu waliomwangalia mtoto. Mama hakuwa na wasiwasi na usalama wa mtoto kwa sababu alijua amemwacha mtoto wa baba mkubwa, binamu au shangazi waliomjali mtoto wake kama ndugu.
Haya mawili, yalifanya suala la malezi kuwa jambo lisilo na changamoto kubwa. Kwamba, baba akiwa kazini, mama alibaki nyumbani. Ikitokea mama naye anawajibika kufanya kazi nje ya nyumbani, ilikuwapo familia tandao kuhakikisha mtoto analelewa ipasavyo.
Hata hivyo, ukaribu wa familia tandao unaendelea kufifia. Kwa sababu kadhaa, imeanza kuwa nadra kuishi na watoto wa ndugu. Kadhalika, akina mama nao wameweza kuingia rasmi katika ajira zinazowalazimu kuwa mbali na nyumbani.
Katika mazingira ya namna hii, wazazi wanakuwa na
changamoto ya kufikiria namna bora ya kuhakikisha mtoto anapata malezi
yanayostahili bila kuathiri kazi ya wazazi nje ya familia. Kwa haraka, zinakuwapo
namna mbili:
Moja, kumtumia mtu mwingine mbali na mama atakayekuwa na jukumu la kumuangalia
mtoto. Mtu huyo anaweza kuwa mama asiye ndugu aliyekubaliana na wazazi kukaa na
mtoto wakati wa mchana; kuajiri msichana atakayeishi na familia kwa lengo la
kumwangalia mtoto; au kupata msaada wa dada mwenye undugu na baba au mama
atakayeweza kukaa nyumbani na mtoto.
Mifano hiyo ni ya huduma zisizo rasmi kwa malezi ya mtoto kutokana na ukweli kuwa hazitolewi na watu wenye ujuzi wa malezi na makuzi ya mtoto. Hata hivyo, ndizo zinazotumiwa na wazazi wengi kwa sababu ya unafuu wake.
Pili, ni utaratibu wa kutumia vituo vinavyotoa huduma rasmi ya uangalizi wa watoto kwa makundi. Kwa utaratibu huu, mama humkabidhi mwanawe kwa mlezi aghalabu mwenye utaalamu wa makuzi kuanzia asubuhi na humfuata mtoto baada ya saa za kazi.
Malezi ya watoto vituoni yako namna mbalimbali. Kuna ya uangalizi wa mtoto kituoni bila natarajio ya elimu rasmi (day care); shule za awali za kutwa ambapo mtoto hupatiwa malezi na elimu (nursery) na shule za awali na msingi za kulala. Zote hizi tunaweza kuziita huduma rasmi za malezi ya mtoto zitolewazo kwenye vituo vinavyotambuliwa kisheria.
Itaendelea…
Christian Bwaya ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Mawasiliano 0754870815 , Twitter @bwaya