KINSHASA, DRC
KANISA Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limeondoa msimamo wake wa awali wa kutotambua matokeo ya uchaguzi wa urais.
Kanisa hilo, ambalo lilikuwa na maelfu ya waangalizi wa uchaguzi wakati wa uchaguzi mkuu wa Desemba
30 mwaka jana, linaamini Rais Felix Tshisekedi hakushinda uchaguzi huo.
Limesema kuwa kufuatia kuapishwa kwa Felix Tshisekedi kuwa rais wiki iliyopita, halitaunga mkono maandamano ya kumpinga.
Mmoja wa wapinzani wa Tshisekedi, Martin Fayulu, anasisitiza kuwa aliporwa ushindi, kutokana na takwimu za Kanisa hilo kuonesha ameshinda kwa kishindo.
Lakini wachambuzi wa mambo wanasema Fayulu hawezi kufika mbali katika madai yake bila uungwaji mkono wa Kanisa la Katoliki, ambalo lina nguvu na ushawishi nchini humo.
Kanisa hilo lilikuwa muhimu katika mandamano makubwa ya kumpinga Rais Joseph Kabila, ambaye ameondoka baada ya kuwa madarakani kwa miaka 18.
Kitendo chake cha kumkabidhi Tshisekedi madaraka ya urais, kilikuwa uhamishaji wa kwanza wa madaraka kwa njia ya amani nchini humo katika kipindi cha karibu miaka 60.