27.7 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

CUF Lipumba wajipanga kuteua bodi mpya

PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, umesema unatarajia kuitisha kikao cha kamati kuu ya chama hicho  waweze kuitisha kikao cha Baraza Kuu ambacho kitateua wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini.

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Saalam, kutengua uteuzi wa bodi ya wadhamini wa chama hicho kwa upande wa Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwa madai kuwa hawana sifa ya kuwa wajumbe wa bodi.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho, upande wa Lipumba, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema  wamekubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu na   wapo kwenye mchakato wa vikao vya juu vya taifa  waweze kufanya uamuzi ikiwamo kuteua wajumbe kama mahakama ilivyoagiza.

“Tupo kwenye mchakato wa kuitisha kikao cha Baraza Kuu ambako muda siyo mrefu tutateua majina ya bodi ya wadhamini na kuwapitisha.

“Kikao hicho pia kitashirikisha viongozi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama sheria inavyotutaka  tuweze kuwa na bodi bora itakayosimamia shughuli za chama,” alisema Kambaya.

Mkurugenzi huyo wa Habari   upande wa Lipumba, alisema   katika kipindi hiki ambacho wako kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho, watahakikisha wanapata bodi mpya mapema iwezekanavyo jambo ambalo linaweza kusaidia shughuli nyingine za chama kuendelea.

Alisema kwa mujibu wa uamuzi wa juzi, bodi zote mbili za Lipumba na Katibu Mkuu wa chama, Maalim Seif Sharif Hamad,  hazitambuliki katika sheria, hivyo basi kufanyika haraka kwa mchakato huo ni muhimu   chama kiweze kuwa na bodi ya wadhamini.

MTANZANIA ilipomtafuta Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande, alisema kwa sasa wanasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya kumtambua Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho au la.

“Kwa sasa tunasubiri uamuzi  wa Mahakama Kuu unaotarajiwa kutolewa Februari 22 mwaka huu wa kumtambua kama Lipumba ni mwenyekiti halali wa chama au laa,”alisema Maharagande.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles