29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Tamisemi yaja na malengo maalumu 14

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

WAZIRI wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ametaja malengo maalumu 14 yaliyopangwa kutekelezwa na wizara yake katika mwaka wa fedha 2019/20.

Jafo aliyataja malengo hayo bungeni juzi, alipokuwa akiwasilisha mapitio, makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka huo wa fedha.

Katika maelezo yake, Jafo alisema wizara hiyo inaomba kuidhinishiwa na Bunge mapato na matumizi ya Sh trilioni 6.207 kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwamo miradi ya maendeleo.

“Katika mwaka wa fedha 2019/20, Tamisemi imepanga kutekeleza kazi maalumu ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya 27 za halmashauri,” alisema Jafo.

Alizitaja halmashauri zitakazojengwa hospitali hizo kuwa ni Karatu, Chalinze, Kondoa, Kongwa, Mbogwe, Biharamulo, Nsimbo, Kigoma, Kakonko, Liwale, Serengeti, Mbeya, Kilombero, Kaliua, Babati, Mvomero, Newala, Sengerema, Kwimba, Madaba, Msalala, Ikungi, Handeni na Mkinga.

Nyingine ni Halmashauri ya Mji Tunduma na halmashauri za manispaa za Sumbawanga na Tabora.

“Vilevile hospitali 67 za halmashauri zilizoanza kujengwa katika mwaka wa fedha 2018/19 zitaendelea na ujenzi katika mwaka wa fedha 2019/20 na zitakamilika Juni, 2019.

“Katika mwaka huo wa fedha, zimetengwa Sh bilioni 46.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizo za halmashauri na lengo jingine ni ujenzi wa vituo vya afya vipya 52 katika baadhi ya kata ambazo hazina vituo ili kuboresha huduma za mama na mtoto na hali ya utoaji wa huduma za afya kwa ujumla.

“Katika mwaka wa fedha 2019/20 zimetengwa Sh bilioni 10.40 kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo vya afya,” alisema Jafo.

ELIMU BILA MALIPO

Katika sekta ya elimu, alisema wataendelea kutekeleza mpango wa utoaji wa elimu msingi bila ada kwa shule za msingi na sekondari hadi kidato cha nne kwani katika mwaka 2019/20 zimetengwa Sh bilioni 288.47 kwa utekelezaji wa mpango huo.

“Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 134.31 zimetengwa kwa shule za msingi na Sh bilioni 154.16 zimetengwa kwa shule za sekondari na ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba 364 za walimu katika shule za msingi kwa mwaka wa fedha 2019/20 zimetengwa Sh bilioni 9.10,” alisema Jafo.

Alisema lengo jingine ni kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo zitajengwa shule za sekondari 26 maalumu za wasichana sawa na shule moja kila mkoa.

MIRADI YA KIMKAKATI

Jafo alisema wizara yake itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati katika halmashauri zilizokidhi vigezo ambapo Sh bilioni 70 zimetengwa kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

“Miradi hiyo ni kufanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 21,525.04 na matengenezo ya makalavati madogo 2,403, madaraja 113, makalavati makubwa 273 na mifereji yenye urefu wa mita 82,627.81 ambapo Sh bilioni 224.94 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo,” alisema Jafo.

WAZIRI MKUCHIKA

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara yake imepanga itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ili utumishi wa umma uendeshwe kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara yake imepanga kuzijengea uwezo taasisi mbalimbali za Serikali katika kuandaa sera zinazozingatia utafiti pamoja na kuandaa sera za kisekta.

“Pia, tutafanya mapitio ya sheria na miongozo mbalimbali ya kiutumishi katika utumishi wa umma kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

“Vilevile tutahuisha miundo ya maendeleo ya utumishi, tutawianisha na kuoanisha mishahara katika utumishi wa umma na pia tutafanya ufuatiliaji kwa kutumia mfumo maalumu na kuhamasisha ujumuishwaji wa masuala maalumu mbalimbali ya kijamii,” alisema Mkuchika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles