29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Siri nzito aliko Rose Muhando

CHRISTOPHER MSEKENA , Dar es Salaam

SIRI nzito imetanda kuhusu sehemu alikohifadhiwa mwanamuziki nyota wa nyimbo za Injili, Rose Muhando, ambaye kwa sasa yupo nchini Kenya alikokwenda kwa huduma ya uimbaji.

Licha ya mwimbaji huyo kuonekana kwa mara ya mwisho Novemba, mwaka huu  kupitia video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii akiwa Nairobi katika Kanisa la Neno Evangelism Centre akiombewa na Mchungaji James Ng’ang’a, lakini hadi sasa  bado hajulikani alipo.

Kutokana na hali hiyo mashabiki na wadau wa muziki wa Injili, wameendelea kuwa gizani na kutokujua sehemu alipo mwimbaji huyo.

Lakini taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinadai kwa sasa anaishi eneo lililofanywa kuwa siri akiendelea kupata matitabu ya ugonjwa ambao nao haujawekwa wazi.

Juhudi mbalimbali zinafanywa na wadau wa muziki huo kujua maendeleo yake na undani wa tatizo lake, lakini zimegonga mwamba kutokana na ugumu wa kumfikia.

Hata hivyo, Desemba 21, mwaka huu kikundi cha wanahabari wanaoutangaza muziki wa Injili Afrika Mashariki kupitia kampeni yao ya ‘Bring Back Rose Muhando’, kiliamua kufanya jitihada za kumfikia msanii huyo.

Kikundi hicho kilimwagiza mmoja wa wajumbe wake aliyepo Mwanza, Fabian Fanuel, kusafiri hadi Nairobi na alifanikiwa kufika Jumamosi kisha Jumapili alianza kufuatilia sakata hilo.

Lakini juhudi za kuonana na Rose hazikuzaa matunda kwa kuwa mwenyeji wake ambaye ni mwimbaji nyota wa Injili nchini Kenya, Annastacia Mukabwa, aliyeonekana naye muda mfupi kabla ya kutoweka, hakutoa ushirikiano kwa kushindwa kutaja hospitali aliyolazwa mwimbaji huyo.

Lakini baadaye Mukabwa aliamua kumjibu Fabian kwa ujumbe wa sauti kupitia mtandao wa WhatsApp, akisema: “Bwana Yesu asifiwe mtumishi, nashukuru Mungu meseji zako nimezipata, samahani kwa sasa sipo maeneo ya Nairobi, nipo mbali huku boda karibia na Uganda katika mkutano na kupatikana kwangu ni kuanzia mwaka ujao ila kwa sasa sitapatikana kwa sababu mikutano yangu tayari ilikuwepo na siwezi kuahirisha.”

Alipoulizwa kama inawezekana kumuona Rose alijibu: “Suala la kumwona Rose sitaki nikudanganye maana pale Rose yupo haruhusiwi mtu yeyote kumwona, yupo katika mikono ya madaktari na yupo ‘very confidential’, kwa sababu hata mimi mwenyewe siruhusiwi kwenda kumwona hadi idhini ya daktari aniambie ni lini nitakwenda kumwona.”

Alisema kutokana na mazingira hayo ni ngumu kumwona na hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kwa kuwa kipindi alichonacho sasa akili yake inahitaji itulie.

“Hahitaji kuongeleshwa na watu wala kuulizwa swali lolote, kuhusu huku nje, nyumbani kwake wala watoto, anahitaji atulie atibiwe hadi daktari atakapoona sawa, basi ubarikiwe nashukuru,” alisema.

Pia wakati umoja wa wanahabari hao ukiajiandaa kesho kwenda Ipagala, Dodoma nyumbani kwa Rose ili kuwajulia hali watoto na familia yake, waimbaji mbalimbali wa muziki huo nao wamekuwa wakipaza sauti kutaka kujua sababu za kuficha sehemu alipohifadhiwa mwimbaji huyo.

Irene Mwamfupe ni miongoni mwa waimbaji nchini waliohoji sababu za kufichwa kwa Rose ambaye ana mashabiki wenye kiu ya kutaka kufahamu hali yake.

“Mimi naona ipo haja ya kwenda Dodoma kwa Rose, tuone ndugu zake, tusikie kama wameridhika na hali hii na kama hawajaridhika tuone namna gani tunaongea nao ikiwezekana hata RB ichukuliwe.

“Tunamuhitaji Rose, hata kama mtu amelazwa tujue amelazwa sehemu gani, kwanini wanaficha, kuna kitu wanachoficha na ni daktari gani ambaye hataki hata watu wajue amelazwa sehemu gani, mimi naona kama kuna kisanaa fulani kinachezwa,” alisema Mwamfupe.

Naye mtayarishaji mkongwe wa muziki Kenya, Eric Mikoomba, aliyejipatia umaarufu kwa kuandaa kazi za waimbaji nyota kama Christopher Muhangila, Bon Mwaitege, Jenipher Mgendi na wengineo, aliliambia gazeti hili kuwa Rose ni mtu mkubwa anayeheshimika nchini humo hivyo hawezi kuachwa akateseka.

“Nyimbo zake zimefanya watu wengi hata majambazi, waasherati wakaokoka kupitia yeye, amefanya kazi kubwa Afrika kwa hiyo lazima mumchukue Rose katika viwango vyake, ni mama wa waimbaji wengi, kweli tuliona mambo yametokea, ameombewa na vitu kama hivyo, lakini wakati hayo mambo yanaendelea shida zake zimeingia katika mikono ya watu wazito.

“Tangu apate shida sijamwona, lakini nimekuwa nikiongea na watu walio karibu naye, wenyewe wanajua yupo wapi, mmoja wao aliniambia Rose yupo salama, anapata matibabu na hana shida yoyote. Anaendelea kuomba Mungu wake na kuandika nyimbo atakazotoka nazo upya na kuwabariki watu.

“Rose hayupo barabarani au analala nje, yupo mahali anashughulikiwa, ana-‘deal’ na watu wazima na nina uhakika viongozi wa Serikali ya Kenya wanajua alipo, hata maaskari wa hapa wanajua yupo wapi, hata huko kwenu watu wakubwa wa Serikali wanajua, Rose hawezi kuteseka na Serikali ya Kenya inamwangalia,” alisema Eric.

Pia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) nalo limeendelea kupata ukakasi wa kufuatilia alipo Rose kutokana na kuondoka nchini bila kibali chao ambacho huwa kinatolewa kwa wanamuziki wanapokwenda nje ya nchi kwenda kufanya shughuli za sanaa.

Rose ni miongoni mwa waimbaji waliofanya mapinduzi makubwa katika muziki wa Injili Afrika Mashariki kwa waimbaji binafsi kupitia rekodi zake nyingi zinazotamba hadi leo zikiwamo ‘Nibebe’, ‘Kamata Pindo la Yesu’, ‘Utamu wa Yesu’, ‘Jipange Sawasawa’, ‘Mteule Uwe Macho’, ‘Nipe Uvumilivu’ na ‘Nakaza Mwendo’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles