RAMADHAN HASSAN, DODOMA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemlilia aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa na Mwenyekiti wa wenyeviti wa chama hicho, Pancras Ndejembi (84).
Ndejembi alifariki dunia jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alikopelekwa juzi kupatiwa matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa, alisema wamepokea kwa masikitiko kifo cha mwanasiasa huyo aliyesema kuwa alikuwa ni mhimili wa ushauri kwa viongozi wa sasa.
“Natoa pole kwa familia, sisi chama mkoa tumepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa kifo chake ukizingatia alikuwa na afya njema, lakini madaktari wamehangaika ila imeshindikana amefariki dunia.
“Yeye kama mshauri wetu mkuu katika mkoa na mmoja wa wazee katika Baraza la Wazee tunakosa mchango wake.
Pia alisema wakati wa uhai wake alikuwa muumini wa kweli wa chama, alikuwa mwadilifu, mwaminifu na mwelekezaji pindi mambo yanapoenda kombo.
Alisema Ndejembi ndiye ambaye ameifanya Dodoma kuwa ngome ya CCM.
“Ameifanya CCM kuwa ngome imara, mara kadhaa alikuwa akiasa tusiyumbishwe, hasa ujio wa vyama vingi vilipoanza yeye alikuwa kinara kwa kuhimiza tushikamane kwa pamoja kukijenga chama chetu na kwa uhakika yeye ametoa mchango mkubwa kiasi kwamba ngome ile sasa imezidi kuwa imara hadi leo,” alisema.
Alisema katika mambo ya siasa anayokumbuka kufanywa na Ndejembi ni kuwaunganisha viongozi wa kisiasa na kuipa heshima Dodoma.
“Ninachokikumbuka ni kule kutuunganisha mkoa kuwa wamoja hasa sisi viongozi, lakini pia kuijengea heshima Dodoma na mara kadhaa amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Dodoma inabaki kwenye kumbukumbu,” alisema.
Pia aliwaomba wana CCM kuwa wamoja katika kipindi hichi kigumu pamoja na kuyaenzi yale mazuri yaliyofanywa na Ndejembi.
“Niwaombe wana CCM tuzidi kumuenzi kwa mema aliyokuwa nayo na juhudi alizozionesha wazi wazi tuziendeleze na juhudi zake za kukijenga chama hapa mkoani na kufanya kuwa ngome basi tumuenzi kwa hilo,” alisema.
Mtoto wa marehemu, Augustino Ndejembi, alisema awali baba yao alilazwa katika Hospitali ya DCMC Ntyuka jijini hapa na kuruhusiwa Desemba 26, mwaka huu.
Alisema walimrudisha nyumbani lakini juzi hali yake ilibadilika na kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na jana asubuhi hali yake ilizidi kuwa mbaya na kisha mauti yalimkuta.
Augustino alisema marehemu atazikwa kijijini kwake katika eneo la Bihawana nje kidogo ya Dodoma pembeni ya kaburi la baba yake.
“Bado tuna ndugu wengi hawajafika Dodoma, kwahiyo siku ya kuzika bado haijajulikana ila atazikwa katika eneo la Bihawana jirani na kaburi la baba yake,” alisema.
HISTORIA
Ndejembi alizaliwa mwaka 1934 Bihawana Dodoma na amewahi kuwa mwalimu wa middle school katika shule za Bihawana.
Pia amewahi kufanya kazi katika Serikali ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kisha kuwa Mkuu wa Wilaya za Tanga, Rombo na Moshi Mjini.
Ndejembi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma kuanzia mwaka 1982 hadi 2007 kisha alimwachia William Kusila, Adam Kimbisa na wa sasa ni Mkanwa.
Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM kwa miaka kadhaa katika utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.