24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mvua yaharibu ekari 300 za mazao Simiyu


DERICK MILTON, BARIADI

MVUA kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali imeharibu zaidi ya ekari 300 za mazao ya pamba, mahindi, mtama na choroko katika Kijiji cha Kilalo, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Mvua hiyo ilinyesha jana kwa muda wa saa moja na nusu huku ikiharibu mashamba mengi, ikiwa pamoja na kuezua paa la nyumba moja mali ya Vumilia Jackson mkazi wa kijiji hicho.

Wakiongea na waandishi wa habari waliofika katika tukio hilo, baadhi ya wananchi ambao mashamba yao yaliathiriwa, walisema kuwa mvua hiyo ilinyesha muda mchache lakini madhara yake yamekuwa makubwa.

Walisema kutokana na mvua hiyo, Serikali iwapatie chakula cha kujikimu kwa kipindi hiki huku wakiendelea na shughuli zao pamoja na kupatiwa mbegu za mazao yanayokomaa kwa muda mfupi.

 “Tunaiomba Serikali itusaidie mbegu za muda mfupi ili turudishie mazao yetu, kwa sasa hatuna kitu, haya mazao ndiyo tulikuwa tunategemea sana kuendesha maisha yetu na ukiangalia tunategemea kilimo hata kusomesha watoto,” alisema Mashili Rozalia.

Naye Vumilia ambaye nyumba yake iliezuliwa na upepo, alisema anaishi yeye na watoto wake saba hivyo ameiomba Serikali kumsaidia sehemu ya kuishi kwa muda.

“Mvua imeleta athari kubwa katika familia yangu, ninaishi na watoto saba baada ya kufiwa na mume wangu mwaka jana, mvua hii imetuacha bila makazi mimi na familia yangu, pia imeharibu chakula,” alisema Vumilia.

Akitoa tathimini ya uharibifu huo, Ofisa Kilimo Kata ya Kilalo, Robert Kipandula alisema mvua hiyo imeharibu mazao ya chakula na biashara, ambayo ni pamba ekari 161, mtama ekari 47 na mahindi ekari 110.5.

“Wakulima walikuwa wamehamasika kulima mazao ya chakula na biashara ikiwamo pamba, mahindi, choroko, mtama, lakini mazao hayo yameharibiwa na mvua ya mawe iliyoambatana na upepo, jumla ya ekari 318 zimearibiwa,” alisema Kipandula.

Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Benjamin Nyasilu alisema mvua hiyo ni janga kubwa kwa wakulima hao kutokana na kuwa na matumaini makubwa kwa jinsi walivyokuwa wamelima.

Alisema wakulima hao wana hali ngumu kimaisha baada ya mazao na vyakula vyao majumbani kuharibiwa na mvua, huku akibainisha kuwa hakuna majeruhi wala kifo kilichotokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles