NEW YORK, MAREKANI
WAZIRI wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Mike Pompeo, anatarajiwa wakati wowote kutoka sasa kutangaza uamuzi wa nchi yake wa kubatilisha makubaliano yanayositisha matumizi ya makombora ya kinyukilia yenye uwezo wa kushambulia kutoka bara moja hadi jingine (INF).
Kwa mujibu wa vyombo vya habari mbalimbali duniani, vimeripoti kwa sauti moja kwamba Marekani imeshawaarifu washirika wake katika Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) kuhusu uamuzi huo.
Makubaliano hayo ya kudhibiti mbio za kutengeneza silaha, yaliyotiwa saini mwaka 1987 kati ya Marekani na Umoja wa Usovieti yamechangia pakubwa katika kumalizika vita baridi.
Mataifa yote mawili yaliahidi kuachana moja kwa moja na makombora ya kinyukilia ya masafa ya wastani. Kwa miaka sasa Marekani imekuwa ikiituhumu Urusi kwenda kinyume cha makubaliano hayo.