Na MWANDISHI WETU-KAGERA
KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, ameanzisha kampeni ya kutokomeza udumavu wa watoto mkoani Kagera.
Kampeni hiyo aliizindua juzi baada ya kukagua kiwanda cha kuchakata nyanya cha Victoria Edibles Ltd kilichopo eneo la Kafunjo, Kata ya Butelankuzi Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Akiwa katika ukaguzi huo, Dk. Bashiru aliwataka viongozi wote wa CCM na Serikali kuendeleza kampeni hiyo ili kupunguza udumavu wa watoto katika Mkoa wa Kagera.
“Kagera ni mkoa wenye vyakula vingi vya asili na ardhi yenye rutuba ya kustawisha mazao mengi kama ndizi, mahindi na mihogo hivyo haipaswi kuwa na ongezeko kubwa la watoto wenye wadumavu,” alisema Dk. Bashiru.
Awali akitoa taarifa kuhusu kiwanda hicho, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jamson Rwekiza, alisema hatua ya kujengwa kiwanda hicho ni utekeleza wa ilani ya uchaguzi ya CCM pamoja na kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli ili kufikia Tanzania ya viwanda.