PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
CHAMA Cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, umesema unatarajia kuitisha kikao cha kamati kuu ya chama hicho waweze kuitisha kikao cha Baraza Kuu ambacho kitateua wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini.
Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Saalam, kutengua uteuzi wa bodi ya wadhamini wa chama hicho kwa upande wa Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwa madai kuwa hawana sifa ya kuwa wajumbe wa bodi.
Akizungumza na wanachama wa chama hicho, upande wa Lipumba, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema wamekubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu na wapo kwenye mchakato wa vikao vya juu vya taifa waweze kufanya uamuzi ikiwamo kuteua wajumbe kama mahakama ilivyoagiza.
“Tupo kwenye mchakato wa kuitisha kikao cha Baraza Kuu ambako muda siyo mrefu tutateua majina ya bodi ya wadhamini na kuwapitisha.
“Kikao hicho pia kitashirikisha viongozi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama sheria inavyotutaka tuweze kuwa na bodi bora itakayosimamia shughuli za chama,” alisema Kambaya.
Mkurugenzi huyo wa Habari upande wa Lipumba, alisema katika kipindi hiki ambacho wako kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho, watahakikisha wanapata bodi mpya mapema iwezekanavyo jambo ambalo linaweza kusaidia shughuli nyingine za chama kuendelea.
Alisema kwa mujibu wa uamuzi wa juzi, bodi zote mbili za Lipumba na Katibu Mkuu wa chama, Maalim Seif Sharif Hamad, hazitambuliki katika sheria, hivyo basi kufanyika haraka kwa mchakato huo ni muhimu chama kiweze kuwa na bodi ya wadhamini.
MTANZANIA ilipomtafuta Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma upande wa Maalim Seif, Mbarala Maharagande, alisema kwa sasa wanasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya kumtambua Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho au la.
“Kwa sasa tunasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu unaotarajiwa kutolewa Februari 22 mwaka huu wa kumtambua kama Lipumba ni mwenyekiti halali wa chama au laa,”alisema Maharagande.