Damian Masyenene – Shinyanga
KATIKA jitihada za kuondoa malalamiko ya utafunaji wa fedha za wakulima na kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga, imeokoa Sh milioni 118,851,957 kutoka vyama vya ushirika na saccoss kati ya Januari hadi Machi, mwaka huu.
Fedha hizo, zilizookolewa ni Sh milioni 107,328,757 zilizookolewa hadi Aprili 17, mwaka huu na Sh milioni 11,523,200 zilizorejeshwa kutoka kwa viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) wilaya za Kishapu na Shinyanga, zikiwa ni fedha za wakulima zilizofanyiwa ubadhirifu, ambapo zitagawiwa kwa wakulima wa pamba hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga jana, Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Hussein Mussa alisema kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, waliendelea kukusanya madeni kwa AMCOS zilizokuwa zinadaiwa baada ya viongozi kufanya ubadhirifu.
Alisema AMCOS 10 kati ya 17, zilikuwa bado zinadaiwa Sh milioni 73,938,080 na wakulima wa pamba.
Alisema viongozi wa AMCOS ya Ibadakuli iliyopo Manispaa ya Shinyanga, walikaidi maelekezo ya kurejesha fedha walizofuja Sh milioni 24,834,000, wamefikishwa mahakamani na kesi ya jinai dhidi yao inaendelea katika mahakama ya wilaya ya Shinyanga.
“Katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2019/2020 (Januari hadi Machi, 2020), tulifanya ufuatiliaji wa madeni uliohusisha uchunguzi wa Chama cha Ushirika Kahama (KACU) na Saccos ya Walimu Kahama, fedha ambazo zilifanyiwa uchunguzi ni Sh 452,395,198 ambazo ni Sh 108,107,816 za Saccos ya walimu na Sh 344,287,382 za KACU, tukabaini chanzo cha madeni ni mikopo ya watu binafsi ambayo chama kiliwakopesha.
“Kwa hiyo hadi kufikia Aprili 17, mwaka huu, tumeokoa Sh 107,328,757 ambapo Sh 4,776,300 ni za saccoss ya walimu Kahama, Sh 102,552,457 za KACU…..kwahiyo jumla tumeokoa Sh 149,355,607 fedha za AMCOS na Saccoss ya walimu Kahama kuanzia Oktoba, mwaka jana, hadi Aprili 17, mwaka huu,” alisema Mussa.
Baada ya kurejeshwa kwa fedha hizo ambazo zilifujwa na na viongozi wa vyama hivyo kwa kutoa mikopo ya watu binafsi na mikopo isiyo rasmi ambayo ilichukuliwa na viongozi na baadhi ya wanachama waliokoma uanachama kwa kustaafu ama kuacha kazi kisha kuondoka na madeni ya chama, Takukuru mkoani hapa inaendelea kuchunguza na kufuatilia madeni ya fedha zilizobaki ambazo ni Sh 62,414,880.
Alisema fedha hizo, ni madeni ya AMCOS za wilaya ya Shinyanga na Kishapu na Sh 241,734,925, ni madeni ya Chama cha Ushirika Kahama (KACU) na Sh 103,331,516 ambazo ni madeni ya Saccos ya walimu wilayani Kahama.
Katika hatua nyingine, taasisi hiyo kupitia dawati lake la kuzuia rushwa inaendelea kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopewa fedha za serikali na ufadhili wa wadau wa maendeleo, ikiwamo miradi saba ya elimu yenye thamani ya Sh 324,238,647 ambayo inaendelea kufanyiwa uchambuzi wa kina katika matumizi yake, pia taasisi hiyo imepokea taarifa 76 zinazofanyiwa uchunguzi huku kesi 24 zikiwa zinaendelea mahakamani.