ZOOM TANZANIA KUIMARISHA BIASHARA MITANDAONI NCHINI

0
546

NA JAMILA SHEMNI, DAR ES SALAAM


BIASHARA ni moja ya nyenzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote. Ukuaji wa uchumi ni pamoja na nchi kujikita katika kuwekeza na kuzitumia vizuri rasilimali zilizopo pamoja na kuviendeleza viwanda.

Si hilo tu, ukuaji wa uchumi ni nyanja pana sana ambayo inahitaji uwajibikaji wa Serikali pamoja na sekta binafsi. Hata makampuni na taasisi binafsi zina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Tanzania ni nchi ya pili kwa kasi ya ukuaji wa uchumi barani Afrika, ambapo kiwango cha ukuaji wa uchumi wake ni asilimia 7.

Mbali na biashara nyingine zinazofanywa na vikundi vya watu au na mtu mmoja mmoja, biashara ya mitandaoni imeanza kuchukua kasi katika miaka ya hivi karibuni na hivyo kudhihirisha wazi umuhimu wake katika ukuaji wa uchumi.

Biashara mitandaoni imewarahisishia wanunuzi wengi wasiokuwa na muda au uvumilivu wa kuzungukia maduka mitaani kusaka na kununua bidhaa mbalimbali.

Uwepo wa mitandao kama Instagram, Facebook, Whatsapp pamoja na tovuti umechangia kurahisisha manunuzi mtandaoni ambao unahusisha kununua na kuletewa ulipo.

ZoomTanzania ni tovuti mojawapo inayojihusisha na biashara mitandaoni kwa kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali nchini.

ZoomTanzania ni tovuti inayoongoza Tanzania kwa matangazo ya biashara kupitia mtandao. Inahusisha biashara 7,500, watumiaji waliosajiliwa zaidi ya 200,000 na ikiwa inatembelewa hadi mara 40,000 kwa wastani wa siku. Ni tovuti inayoaminika zaidi katika kuunganisha wanunuzi na wauzaji nchini Tanzania.

Katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuijenga Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,  ZoomTanzania imedhamiria kuendelea kufanya mageuzi makubwa kuhakikisha Watanzania wanatumia teknolojia ya kisasa kujikwamua kiuchumi na hivyo kukuza viwanda nchini na kuajiri  Watanzania ambao watakuwa viongozi kwenye viwanda mbalimbali.

Mageuzi hayo ni pamoja na kutoa elimu kwa Watanzania kuhusiana na tovuti ya Zoom na fursa zilizopo ili kujikwamua kiuchumi.

Ikiwa ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kushiriki katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, imejidhihirisha wazi jinsi gani imekua na iko tayari kuwasaidia Watanzania kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika Maonyesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yanayoendelea Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZoomTanzania, Mili Rughani (pichani) anasema: “Kitendo cha sisi kushiriki katika Maonyesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, yakiwa ni maonyesho ya kwanza kushiriki tangu kuanzishwa kwa kampuni hii mwaka 2009, inaonyesha ni jinsi gani tumekua na kujitangaza kimataifa na kuleta uelewa kuhusiana na Tanzania kuhamia digitali.

“Dhana ya kuhamia digitali ikiwa bado ni dhana mpya Tanzania, tumejikita kuwapa uelewa Watanzania kuielewa dhana hii. Hii ni njia pekee ambayo unaweza kufanya biashara na kupata mrejesho papo hapo.

“Ni imani yetu kupitia maonyesho haya yatatujengea uaminifu na kutuimarisha zaidi katika kupanua wigo hadi kufikia kimataifa,” anasema.

Anasema mbali na kwamba kuna tovuti na mitandao mbalimbali inayofanya biashara kwenye mitandao, lakini wao wanaamini Zoom wanatumia teknolojia mpya ambayo ni ya kisasa, ya kwanza na ya kipekee Afrika Mashariki.

Akizungumzia dhana ya Tanzania ya viwanda, Ofisa Mtendaji Mkuu huyo anasema Zoom inawapa wanunuzi na wauzaji mwanya na fursa ya kufanya miamala mbalimbali ya biashara kwenye mitandao na hivyo ni njia mojawapo ya kuhakikisha biashara zinakua na  viwanda vinakua na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

“Ni dhahiri kwamba, ukuaji wa biashara unaenda sambamba na ukuaji wa biashara. Hivyo sisi tuna jukumu la kuhakikisha tunawaunganisha wanunuzi na wauzaji kupata bidhaa bora na hivyo kufikia lengo la Serikali la kufikia uchumi wa kati kwa kuhakikisha biashara zinakua na kuviendeleza viwanda nchini,” anasema.

Ofisa Mtendaji Mkuu huyo anakwenda mbali zaidi na kusema kwamba, tangu achaguliwe kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZoomTanzania, anaamini sana kwa kuwawezesha Watanzania kuwa viongozi bora katika siku zijazo.

“Hatua ya kwanza tumeanzisha programu ambapo vijana wa Kitanzania watapata fursa ya kufanya kazi katika sekta yenye nguvu ambayo inakua haraka sana. Pili, tumeanzisha bidhaa mpya (dhahabu na fedha), bidhaa hizi kwa mara ya kwanza zimeathiri uwezo wa kununua wa watumiaji na ZOOM tayari imeona ukuaji wake,” anasema.

Naye Meneja Masoko wa ZoomTanzania, Legendo Khalfan, anasema mwitikio wa Watanzania katika wa Maonyesho ya Sabasaba  ni mkubwa na kwamba watu wameanza kuelewa jinsi tovuti inavyofanya kazi.

“Asilimia 90 ya Watanzania wanaokuja kwenye banda letu Sabasaba wanafurahia huduma zetu na wako tayari kufanya kazi na sisi,” anafafanua.

Anasema Zoom imejipanua zaidi ambapo sasa wameamua kuonana ana kwa ana na wateja na hivyo kuwapa elimu ya jinsi gani wanaweza wakafikiwa na wateja wengi kupitia tovuti yao.

Akiutaja utapeli unaofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao kama changamoto kwao na kuwaondolea uaminifu Watanzania, anasema hiyo ni changamoto kubwa, hivyo kuna kampeni kubwa inakuja kwa ajili ya kueneza ujumbe kwa jamii.

“Ni kweli utapeli upo kwa baadhi ya mitandao, ila sisi tupo tofauti na tumekuja kivingine, tunataka Watanzania wajenge imani kupitia sisi kwamba biashara kupitia mitandao inawezekana na inaleta tija,” anasema.

Kwa upande wa wauzaji na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali kupitia mitandao, wameeleza kufurahishwa na huduma zitolewazo na ZoomTanzania na wamedhamiria kuitumia ili kuendeleza maisha yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here