31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto, polisi wabanana mauaji Kigoma

            ELIZABETH HOMBO Na EDITHA KARLO

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, limemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kufika mkoani humo na kuthibitisha madai yake kuhusu mauaji ya wananchi zaidi ya 100 katika Wilaya ya Uvinza mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki , Zitto alidai kuwa mauaji hayo yalitokea katika tukio la mapigano kati ya polisi na Wanyantuzu wilayani Uvinza, takribani siku 11 zilizopita.

Kiongozi huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo, alidai kuwa katika tukio hilo, mbali na wananchi 100 kupoteza maisha pia askari wawili wanadaiwa kufariki dunia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno, amesema Zitto amezungumza upotoshaji mkubwa na kwamba anatafuta umaarufu, hivyo apuuzwe.

Alisema ni wananchi wawili na askari wawili tu ndiyo wamepoteza maisha na si 100 kama alivyodai Zitto.

Akizungumza jana ofisini kwake mkoani Kigoma, Kamanda Ottieno alimtaka mbunge huyo kufika mkoani humo na kuthibitisha taarifa anazozitoa kuhusiana na tukio hilo na kwamba awapeleke polisi katika eneo hilo ambalo amedai wananchi hao wameuawa na kupigwa na polisi.

“Tunamtaka Zitto aje Kigoma ili athibitishe taarifa anazozitoa na atupeleke kwenye hilo eneo ambalo wananchi wameuawa kwa kupigwa na polisi na atuonyeshe hayo makaburi,”alisema kamanda huyo.

Alisema taarifa za Zitto ni za upotoshaji mkubwa na zinalenga kutengeneza uhasama mbaya baina ya Jeshi la Polisi na raia.

Alisema Jeshi la polisi likiwa katika harakati ya kuwahamisha wafugaji katika eneo la Nalco katika Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, askari wawili na wananchi wawili waliuawa.

Kamanda huyo alitaja majina ya askari waliofariki dunia ni Ramadhani Mdimi na Mohamed Nzengwe huku wananchi wawili wakiwa ni Sau Deus na Adam Baraka na majeruhi watano.

Alimtaka mwanasiasa huyo kutumia vizuri majukumu ya siasa kwa kuwahamasisha wananchi wapate maendeleo na si kutumia majukwaa kutoa taarifa za uongo.

Kamanda Ottieno alisema Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua atakayejihusisha na upotoshaji wa suala hilo au jambo lolote.

MTANZANIA ilipomtafuta Zitto kuhusiana na wito huo, alisema bado hajaupata na kwamba katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari jambo la kwanza alitaka polisi kutoa taarifa kwa umma kuhusu mauaji hayo.

“Sijapata wito huo, kauli yangu ilikuwa wazi kabisa kuwa polisi watoe taarifa kwa umma. Wametoa taarifa ambayo hawakuwa wametoa. Tunatafakari,”alisema.

Alipouliwa anatafakari wito wa polisi au taarifa iliyotolewa na jeshi hilo, alisema chama chake kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na kitaweka wazi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Zitto alisema wiki iliyopita yalitokea mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Mto Malagarasi, Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka aliuawa na wanaodaiwa kuwa ni wananchi.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yote yanayojiri huko Uvinza tangu kuuawa kwa askari polisi wetu. Tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno.

“Kwani tunaambiwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi limekalia kimya suala hili, pamoja na IGP kutembelea eneo hilo la maafa. Haiwezekani kamwe tukio kubwa namna hii kutokea halafu Serikali ibaki kimya bila kutoa maelezo yoyote kwa wananchi. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanywa ili kutambua nini kimetokea pale Mpeta.

“Kwa sasa tunaitaka Serikali ieleze nini hasa kimetokea, maelezo hayo yawe ya kina na yawe ya ukweli. Chama chetu kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na tutaweka wazi taarifa husika,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles