27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto, Bashe watua Takukuru

Untitled-1*Ni kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya wabunge

*Wahojiwa kwa saa mbili sababu za kujiuzulu kwao

 

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

OFISI ya Bunge kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), zimeendelea kuwabana wabunge mbalimbali ili kuweza kubaini waliohusika na kupewa rushwa kutoka mashirika ya umma.

Kutokana na hatua hiyo, jana wabunge wawili ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, waliitwa kwenda kutoa maelezo Takukuru.

Walioitwa jana na kuhojiwa kwa zaidi ya saa mbili ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM).

Licha ya wabunge hao kuwasilisha barua za kujiuzulu kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kama njia ya kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wenyeviti na makamu wao, lakini bado wamejikuta wakiitwa kama lengo la kusikiliza maelezo yao.

Hadi kufikia jana, tayari Takukuru imewahoji zaidi ya wabunge saba, wakiwamo wale wanaotajwa kuhusika na kuchukua mlungula huo pamoja na wale ambao hawajatajwa.

Akizungumza na MTANZANIA, Zitto alikiri kuitwa na Takukuru na akasema kuwa amewapa ushirikiano kwa kile anachokifahamu.

“Nafurahi wito wetu wa uchunguzi umechukuliwa kwa uzito unaostahili na tutatoa ushirikiano wote kwa vyombo vya uchunguzi ili kumaliza zoezi hili kwa haraka na kwa ufanisi,” alisema Zitto.

Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo na Takukuru, Zitto aliandika katika mtandao wa Facebook kwamba kama taasisi za uwajibikaji zikifanya kazi vizuri, ufisadi utaondoka.

“Taasisi za uwajibikaji zikifanya kazi zake vizuri, tutaondoa ufisadi wa kimfumo na mfumo wa kifisadi nchini. Tuweke tu mazingira ambayo kila mtu anawajibika kwa matendo yake na kuua ‘impunity’.

“Mchakato unaoendelea sasa unajenga imani kwenye taasisi. Itasaidia sana kupunguza majungu na hisia. Itasaidia sana kukamata wakosaji na kuzuia makosa hayo kwenda mbele. Huko ndio kujenga taasisi na kubadili mfumo,” alisema.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, alisema uchunguzi wa vyombo vya dola ni moja ya njia mwafaka ya kuhakikisha kila linalosemwa linakuwa na ukweli na pale ambapo suala limezushwa, itajulikana na wazushaji hatimaye wataacha.

Baada ya kuhojiwa Zitto, ilifuata zamu ya Bashe, ambaye naye alihojiwa kuhusu suala hilo la rushwa.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Bashe alithibitisha kuitwa na maofisa wa Takukuru baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Ofisi ya Bunge.

“Ni kweli nimeitwa na nimehojiwa, kwanza nilichojifunza Takukuru walianza uchunguzi wa suala hili kabla ya umma kujua. Na uchunguzi wao utasaidia kujenga taswira ya Bunge maana kumekuwa na dhana nyingi dhidi ya wabunge na Bunge letu,” alisema Bashe.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa pamoja na hatua hiyo, wameulizwa sababu ya kujiuzu kwao ujumbe wa kamati na namna wanavyofahamu kuhusu tuhuma za rushwa kwa wabunge.

 

BASHE, ZITTO WALIVYOJIUZULU

Wabunge hao wawili walimwandikia barua Spika ya kuomba kuachia ngazi kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwenye kamati yao.

Katika barua yake ya Machi 22, mwaka huu, Bashe alimwandikia Spika akieleza kuwa kuna tuhuma nzito zilizochapishwa katika vyombo vya habari zikieleza kuwapo kwa ufisadi katika kamati za Bunge jambo ambalo linaweza kuharibu sifa ya kamati hizo, Bunge na wabunge binafsi, hivyo uchunguzi wa kina ufanyike na hatua kali zichukuliwe dhidi ya watakaobanika kuhusika.

“Ninajiuzulu ujumbe wa kamati ninayohudumia sasa ili kupisha uchunguzi. Bunge litaje wahusika hata nikiwa mimi ili kutunza heshima ya kamati na taasisi. Ni vigumu kuhudumia wakati umma unaitizama kamati kama ‘corrupt’, ili niweze kutimiza wajibu wangu ni vizuri kujiridhisha uhusika wa kamati na namna tulivyohusika,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Bashe.

Wakati Bashe akiandika hayo, Zitto katika barua yake ya Machi 22, mwaka huu aliyoipa kichwa cha maneno ‘tuhuma za ufisadi dhidi ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii,’ aliandika kuwa ameamua kujiuzulu ujumbe wa kamati anayohudumia ili kupisha uchunguzi dhidi ya vitendo vya ufisadi vya baadhi ya wabunge vilivyoripotiwa na gazeti la MTANZANIA.

“Tuhuma hizi ni nzito sana na zinaweza kuharibu kabisa sifa ya Bunge na kamati zake, kwa vyovyote vile tuhuma hizi zimeharibu sifa ya wabunge binafsi. Kwa barua hii naomba Bunge liagize uchunguzi wa kina na kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekutwa kahusika.

“Kumekuwa na tuhuma za mara kwa mara dhidi ya wabunge nyakati tofauti. Kufanyika uchunguzi na …….. kuchukua hatua ni chanzo cha mwendelezo wa tuhuma za namna hii. Nashauri kuwa safari hii jambo hili lichukuliwe kwa uzito unaostahili,” alisema Zitto katika barua yake kwenda kwa Spika.

Machi 23, mwaka huu, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alifanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge, huku akiwaondoa wenyeviti na makamu wenyeviti watano katika kamati walizokuwa wakiziongoza.

Katika mabadiliko hayo yaliyowagusa jumla ya wabunge 27, Spika Ndugai ametoa maelekezo ya kujazwa kwa nafasi zilizoachwa wazi za wenyeviti na makamu wenyeviti walioguswa na panga pangua hiyo na kusititiza utekelezaji wa maagizo yake kuanza mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Bunge, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Umma, uamuzi wa Spika umezingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuundwa kwa kamati za Bunge Januari, mwaka huu.

Wenyeviti walioguswa na rungu la mabadiliko yaliyofanywa na Spika Ndugai ni Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini aliyehamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), aliyehamishiwa kamati ya Katiba na Sheria.

Mwingine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa (CCM), ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ambapo amejikuta akihamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Makamu wenyeviti walioondolewa kwenye kamati zao ni Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Sambamba na hao, wabunge wengine 22 nao wamehamishwa kutoka kamati walizokuwa kwenda katika kamati nyingine.

MTANZANIA lilikariri taarifa za kibunge zilizoeleza kuwa taasisi zilizofikiwa na wabunge wanaotuhumiwa kuombwa rushwa kuwa ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles