Na Editha Karlo, Kigoma
KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka wananchi na wanasiasa mkoani Kigoma kuunga kwa pamoja kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ili kuweza kupata viongozi watakaoletea maendeleo.
Â
Zitto ameyasema hayo leo Juni 3,2023 katika uwanja wa barafu kwenye mji mdogo wa Mwandiga alipokuwa akimtambulisha aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum CUF, Kiiza Mayeye ambaye amejiunga na ACT Wazalendo.
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo ambaye amewahi kuwa mbunge kwa miaka 15 kwenye majimbo mawili tofauti mkoani Kigoma amesema wakati wa harakati za kisiasa mambo mengi yanatokea ambayo wakati mwingine yanawakwaza watu ingawa inaweza kuwa bila kukusudia hivyo akachukua nafasi hiyo kuomba radhi na kuomba asamehewe kwa yote yaliyotokea.
Zitto amesema wananchi na viongozi wa kisiasa mkoani Kigoma wanapaswa kuungana ili kusimamia maslahi ya wananchi kwa pamoja badala ya kutengana kila mmoja kupigania jambo hilo kivyake hatua ambayo inawagombanisha wao kwa wao.
Aidha, Zitto ameongeza kuwa ili kuikabili CCM wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuifanya ACT kuwa na nguvu ya kusimamia mchakato huo.
Katika mkutano huo Kiongozi huyo wa ACT aliwapokea makada wawili wa CCM akiwemo aliyewahai kuwa Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kigoma, Kalembe Masudi ambaye aliwahi pia kuwa diwani wa kata ya Herembe Wilaya ya Uvinza sambamba na kumpokea Lumu Mwitu aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM kata ya Mwanga Kusini na Mwenyekiti wa Mtaa.
Pamoja na mambo mengine katika mkutano huo Kiongozi huyo amezungumzia mchakato wa katiba mpya na kuridhia uendelee ingawa ametaka kuwepo kwa sheria ya uchaguzi ili kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi ambayo Katiba mpya inayopiganiwa iweze kutambua hilo.
Akizungumza katika mkutano huo Mwanachama huyo mpya wa ACT Wazalendo, Kiisa Mayeye amesema hakukurupuka kama ambavyo amekuwa akishambuliwa kwenye mitandao kwa mpango wake wa kujiunga na ACT na badala yake alibainisha kuwa alifanya utafiti na kufikia uamuzi huo.
Mayeye amesema amesema kuwa alisoma na kuzielewa sera za ACT na namna walivyojipanga hivyo ameona dhamira yake ya kuwapigania wananchi wa mkoa Kigoma itatimia kupitia chama hicho na kwamba usajili unaofanywa na ACT kwa sasa utakipa ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.
Katika hatua nyingine, mwanachama huyo mpya wa ACT amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza demokrasia kwa vitendo kwa kuruhusu mikutano ya siasa na kuongeza kuwa kiongozi huyo ataacha kumbukumbu kubwa iwapo atatekeleza na kuumaliza mchakato wa katiba mpya kabla uchaguzi mkuu wa 2025.