MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amemshangaa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, pamoja na kamati yake kwa kushindwa kumchukulia hatua Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, licha ya kushindwa kutekeleza agizo la Mahakama.
Kauli hiyo aliitoa bungeni mjini Dodoma jana alipokuwa akichangia taarifa ya utekelezaji wa kazi za Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa mwaka 2014.
Katika taarifa hiyo ilielezwa kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa kutekeleza amri ya Mahakama Kuu iliyoitaka wizara hiyo kutangaza katika Gazeti la Serikali, kuhusu kuanza kutoa tozo mpya kwa hoteli za kitalii zilizoko katika hifadhi za taifa na kusababisha hasara ya Sh bilioni 80 kwa Serikali.
“Katika nchi hii tumekuwa tukilalamika kwamba Serikali inapoteza mapato katika mazingira yasiyokubalika. Leo, hapa kamati imesema Waziri wa Maliasili na Utalii ameshindwa kutekeleza agizo la mahakama na kuisababisha Serikali ikose mapato ya Sh bilioni 80.
“Pamoja na kupoteza fedha hizo, mwenyekiti wa kamati ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwawajibisha viongozi wasiowajibika, katika wizara hii amekuwa na kigugumizi, kwa nini?
“Nakubaliana na kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Lema (Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini) kwamba hapa kuna mapacha watatu, yaani waziri, mwenyekiti wa kamati na waziri kivuli.
“Kwa hiyo kama waziri umeshindwa kutangaza katika Gazeti la Serikali, ikifika leo jioni (jana) uwe umeandika barua ya kujiuzulu kwa rais kwa sababu umeshindwa kazi,” alisema Zitto.
Awali akiwasilisha taarifa hiyo, Lembeli alisema kuwa hatua ya Wizara ya Maliasili na Utalii kushindwa kutekeleza amri ya Mahakama Kuu iliyoitaka wizara hiyo kutangaza katika Gazeti la Serikali kuhusu kuanza kutoa tozo mpya kwa hoteli za kitalii zilizoko katika hifadhi za taifa imesababisha hasara kwa taifa.
“Tarehe 12 Septemba mwaka 2014 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ilitoa hukumu ya kesi iliyokuwa imefunguliwa na baadhi ya wamiliki wa hoteli zilizoko katika hifadhi za taifa dhidi ya TANAPA.
“Tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo mwaka 2011 hadi Septemba 2014, TANAPA imepoteza karibu Sh bilioni 80 kutokana na kukosekana kwa malipo ya tozo hiyo,” alisema Lembeli.
Kutokana na hali hiyo, alisema kamati iliitaka wizara hiyo kutangaza tangazo hilo katika Gazeti la Serikali ifikapo Januari 28 mwaka huu.
Pamoja na hayo, alisema kamati hiyo inaitaka Serikali itoe maelezo ni kwa nini imeshindwa kutekeleza amri hiyo ya mahakama bila sababu za msingi.