23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

ZITTO ATAKA MWIJAGE AJIUZULU, SPIKA ATAKA MAWAZIRI WASAFIRI

GABRIEL MUSHI NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA


MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe  (ACT- Wazalendo), amemtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ajiuzulu kwa kushindwa kuinusuru wizara yake huku Spika Job Ndugai, akishauri waziri huyo aombewe kwenye mamlaka ili asafiri nje ya nchi.

Awali Zitto akichangia hotuba ya wizara hiyo, alisema Mwijage akubali kujiuzulu kwa kuwa ameshindwa kuinusuru wizara hiyo ambayo sasa inapoteza zaidi ya Sh bilioni tatu kwa siku katika bidhaa zinazotakiwa kusafirishwa nje ya nchi.

Zitto alisema bidhaa za dengu, mbaazi, choroko na giligilani zingeiwezesha Serikali kupata fedha za kigeni ambazo zingetumika kununua mafuta ya kula na sukari.

“Wizara ya viwanda na biashara tumepoteza Dola za Marekani bilioni moja katika kipindi cha miezi 24 ni sawa sawa na kupoteza kila siku Sh bilioni tatu kwa mwaka uliopita.

“Bado upo hapa kwanini usi-quit (jiuzulu)! umeshindwa kazi, huwezi kuendesha Wizara ya Viwanda na Biashara kama Tamisemi, wizara hii inahitaji diplomasia na kwenda nje kutafuta masoko,” alisema.

Alisema leo inashangaza kuona Tanzania inaagiza mafuta gafhi ikiwamo mawese ambayo yanawezekana kuzalishwa katika mikoa ya Kigoma, Dodoma na Singida.

“Kiongozi Mkuu wa Malaysia ni rafiki wa Mwalimu Nyerere, nenda kule kazungumze naye huwezi kujidanganya na viwanda vya cherehani, biashara ina nguvu. Kwa mfano Waziri Mkuu wa India anatokea eneo linaloitwa Bujarati wakati asilimia 90 ya wahindi waliopo nchini wanatokea eneo hilo pia, zungumza nao,” alisema.

Alisema licha ya kuwapo kwa miradi ya Liganga na Mchuchuma ambayo imanza tangu mwaka 2000, Serikali imeshindwa kuiwekea mikakati na sasa inalazimika kuagiza malighafi ikiwamo vyuma kutoka China na Uturuki kwa ajili ya ujenzi wa reli na viwanda vya nondo nchini.

“Spika wewe ni mbunge, toka mwaka 2000 tunazungumza Mchuchuma na Liganga. Sijui sisi ni watu wa namna gani. Tunaongea vitu vilevile miaka yote tunakumbushana hamna kitu kinachoendelea. Leo vyuma vya ujenzi wa reli vinatoka Uturuki, China wakati tungeweza kuwauzia hata Kenya na Zambia ambao wanajenga reli.

“Mwaka 2016 Serikali ilikuja na mpango unaoitwa C2C (Cotton to Clothes), nimeangalia hotuba ya waziri hata kulizungumza neno hilo ameona aibu, unaondoaje umaskini bila viwanda vya nguo? nchi kama Uingereza ndio walifanikiwa huko,” alisema.

Alisema mauzo bidhaa za Tanzania nje kama vile Japani  yameshuka kutoka Dola za Marekani milioni 140 hadi 75.

“Lakini tumeshindwa kuuza mbaazi India, waziri amesema alikwenda India, Waziri … biashara ni diplomasia, huwezi kuzunguka na viwanda vya cherehani hapa ndani sambamba na naibu wako! biashara ya kimataifa ndio yenye nguvu.

“Kwa mfano Makamu wa Rais alikuwa London na Waziri Mkuu wa India Narenda Mod alikuwa London vilevile lakini mmeshindwa kupata nafasi ya kuzungumza naye kutatua tatizo la mbaazi. Mbaazi bei imeporomoka kutoka Sh 3000 mpaka 150 kwa kilo moja, watu wanalia mbaazi zipo ndani,” alisema.

Alsema katika kipindi cha mwaka 2016, mazao ya mbaazi, choroko na giligilani zilikuwa zinaipatia Serikali dola za Marekani milioni 224 kwa kuuza India, mwaka 2017 ziliporomoka hadi dola za Marekani milioni 131 na mwaka 2018 zitafikia dola za Marekani milioni 75.

Spika: Tuwaombee kwenye mamlaka mawaziri wasafiri

Baada ya Zitto kuhitimisha mchango wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai alikiri kuguswa na mchango huo na kusisitiza kuwa ni kweli wawaziri inabidi wasafiri.

“Waziri wa biashara hawezi kukaa na sisi hapa, lazima aende, tumwombee popote pale kwenye mamlaka lazima asafiri, maana bidhaa zetu tutauza Kongwa! kuna soko huko? Waziri wa utalii lazima asafiri apige mawingu huko na wengine huko… ndio ukweli jamani, sisi wabunge lazima tuwasemee,” alisisitiza Ndugai.

Naye Mbunge wa Babati Vijiji, Vrajilal Jituson (CCM), alisema Serikali inapoteza kodi nyingi katika vinywaji vya pombe kali.

Alisema Serikali lazima ihakikishe inapata kodi sahihi pamoja na kuanzisha viwanda vya kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Ni muhimu Serikali ikapanga kodi sahihi ili isiendelee kupoteza mapato,” alisema

Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema), alisema Serikali ni lazima iangalie namna bora ya kufufua mashine ambazo zipo katika viwanda mbalimbali nchini kwa kuwa nyingi zimechakaa.

Alisema inashangaza kuiona serikali ikiweka kipaumbele zaidi kwenye miradi mipya ilihali miradi ya awali ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa sekta ya viwanda nchini ikiendelea kupewa kisogo.

“Kwa mfano miradi ya Liganga na Mchuchuma, ni miradi ya siku nyingi lakini inashangaza kuiona serikali haitoi kipaumbele kwa miradi hii iliyoanza tangu awamu ya tatu na badala yake sasa ndio inalipa fidia,” alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Shamsia Aziz Mtamba (CUF) aliiomba Serikali kueleekeza nguvu zaidi katika miradi ya gesi asilimia kutatua tatizo la umeme vijijini utakaosaidia vijana kujiajiri.

“Naishauri Serikali iwekeze kwenye uzalishaji wa gesi. Pia ipunguze kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili tuwasaidie wananchi kujikwamua kiuchumi,”alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Kiteto Koshuma alishangazwa na kitabu cha waziri kutokuwa na sehemu inayozungumzia viwanda vya nguo.

Koshuma alisema umaskini tulionao unasababishwa na kubinafsishwa kwa viwanda 146 vilivyokuwepo nchini.

“Leo tupo wapi, tunaenda wapi, Mwatex iliajiri wafanyakazi 3500 ipo wapi, Mutex ipo wapi. Viwanda vingi impact yake haionekani,” alisema.

Koshuma pia aliiomba Serikali itoe tozo ya asilimia 18 katika viwanda vya nguo.

Kwa upande wake Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama, (CCM) alisema ili sera ya viwanda iweze kukamilika ni lazima Serikali iwekeze katika chuma.

“Tuna utajiri mkubwa katika kutoka Liganga na Mchuchuma lakini hatuitumii,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,303FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles