IKIWA ni takribani miaka mitatu tangu Zitto Zuberi Kabwe ahame kutoka Chadema kwenda ACT, bado mijadala haikukoma dhidi yake.
Zitto kuendelea kujadiliwa baada ya kutimkia ACT ni kutokana na mchango wake katika kuijenga Chadema ambapo baadhi ya wananchi wanadai kuwa huwezi kuzungumzia nguvu ya chama hicho ukampuuzia mwanasiasa huyu ambaye kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja alisababisha vijana wengi kunogewa na mabadiliko.
Mwaka 1992, Zitto akiwa na umri wa miaka 16 alijiunga na Chadema mara baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi na baadaye mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 29, alifanikiwa kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia bungeni kupitia chama hicho akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Akiwa bungeni Zitto amekuwa kivutio kutokana na misimamo yake katika kutetea maslahi ya umma ikiwamo kupinga ufisadi na kubadilisha baadhi ya sheria mbovu.
Hata hivyo mbali na kuipigania Chadema ndani na nje ya Bunge bado Zitto alifukuzwa kutokana na kilichotafsiriwa utovu wa nidhamu.
Zitto akihisiwa kuwa kibaraka wa CCM, ili kuuzika upinzani, lakini inasemekana mgogoro uliompa talaka msomi huyu wa uchumi ni kukimezea mate kiti cha mfalme.
Ni wazi mgogoro huu uliosababisha Zitto kutimkia ACT 2015 mwaka ambao kimsingi ulikuwa ni wa Uchaguzi Mkuu, kwa kiasi fulani ulidhoofisha upinzani.
Ulidhoofisha upinzani kwa maana ya kwamba pamoja na kuwapo umoja wa Ukawa lakini ikumbukwe ACT haikuwamo katika umoja huo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Dk. Patrick Asingo wa Kenya ni kwamba vyama vya upinzani Afrika vimekuwa vikishindwa kuviondoa vyama tawala kutokana na kukosa ushirikiano.
Dk. Asingo ameitumia Kenya ambapo vyama vya upinzani kwa kukosa umoja vilishindwa kuiondoa KANU katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1992 na 1997.
Aidha msomi huyu kwa kuonesha nguvu ya umoja ndani ya upinzani, amevitumia vyama vya NAK na LDP, vilipojitambua na hatimaye kuunda umoja wa NARC, mwaka 2002 vilifanikiwa kuing’oa KANU madarakani.
Dk. Asingo katika utafiti wake ameonesha kuwa si tu umoja peke yake wa upinzani hufanikisha kuondoa chama tawala, bali pia na sababu nyingine kama Serikali kulemewa na vitendo vya ufisadi huku pengo la maskini na matajiri likizidi kuongezeka.
Zitto akingali Chadema aliwahi kuhojiwa na Jamii Forum mwaka 2012 kwamba Je, anaona tofauti ipi ya msingi kati ya CCM na Chadema ambapo alijibu kwa kusema: ‘‘CCM imeshindwa kupambana na adui ufisadi, Chadema tunapambana na tutapambana na ufisadi kwa nguvu zetu zote.’’
Majibu ya Zitto yalikuwa sahihi kwani katika miaka ya nyuma upinzani ulikuwa ukijiongezea umaarufu kwa kutembelea kete ya ufisadi uliokuwa umeota mizizi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
La kujiuliza kama upinzani unaozidi kugawanyika ulikuwa unazaa matunda kutokana na chama dola kulemewa na ufisadi, leo hii JPM anaendelea kusifika kwamba anawapa kichapo mafisadi, Je nini matokeo yake?
Haitoshi Zitto aliwahi kusema kuwa ndani ya Chadema kuna utaratibu mzuri wa kujieleza hivyo yeye binafsi, Dk. Slaa, Mbowe na Prof. Mkumbo ni Presidential Materials, lakini sasa hivi miongoni mwao hawako huko, nini hatima yake?
Wakati Zitto mwenye kuonekana bado anajikongoja kisiasa akisema katika Uchaguzi Mkuu ujao hagombei ubunge bali Urais, pamekuwapo na tetesi kuwa ACT inajiunga kinyemela na Ukawa ili kuimarisha upinzani, lakini la kujiuliza ni Je atakubaliwa kupewa uzito ili akawe mzito Magogoni?
Ndugu Zitto Kabwe
,