ZITTO ALIA NA SUMATRA KUTOA VIBALI

0
521
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo)

 

 

Na Ramadhan Hassan,

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), amehoji kuhusu Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kutoa vibali vya usafiri kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika.

Akiuliza swali jana bungeni kwa niaba ya Zitto, Mbunge wa Buyungu, Bilago Kasuku (Chadema), alitaka kujua ni kifungu gani cha sheria kinaipa mamlaka Sumatra kutoza ushuru kwa wavuvi na wakati huo huo haifanyi hivyo kwa matrekta ya kilimo.

“Je, Serikali haioni kuwa inadidimiza wavuvi kwa kuwarundikia tozo nyingi na kuwafanya waendelee kuwa masikini?” alihoji Kasuku.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, alisema mamlaka hiyo haitoi vibali wala haitozi ushuru kwa vyombo vya usafiri majini nchini, ikiwa ni pamoja na wavuvi wa Ziwa Tanganyika.

Waziri Ngonyani, alisema Sumatra inalo jukumu la kukagua ubora wa vyombo vya usafiri majini, ikiwa ni pamoja na vya uvuvi na kutoa cheti cha ubora.

“Moja ya majukumu ya msingi ya Sumatra katika vyombo vya usafiri na vya uvuvi, ni kuhakikisha vyombo hivyo ni salama kabla ya kuanza kufanya shughuli za majini,” alisema.

Ngonyani alisema Serikali haikusudii kudidimiza wavuvi  wala haijawarundikia tozo nyingi ambazo zitawafanya wawe masikini, bali inawahakikishia mazingira salama kwa kufanya shughuli zao za uvuvi,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here