24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO AITAKA SERIKALI ITANGAZE BAA LA NJAA

zitto-kabwe

NA MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameitaka Serikali itangaze rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria.

Zitto alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Nkome mkoani Geita kupitia ACT-Wazalendo.

“Hali ya chakula nchini si nzuri. Wananchi mmeshuhudia namna bei za vyakula zinavyopanda kila siku. Bei ya sembe sasa kilo moja imefikia shilingi 1,600 pale Morogoro, kilo moja ya mchele ni shilingi 1,500, maana yake leo ugali na wali imekuwa bei inafanana. Gharama za maisha zitaendelea kupanda kutokana na uhaba wa chakula kuwa mkubwa.

“Kwanini hali ya chakula inazidi kuwa mbaya? Ni kwa sababu ya uamuzi mbovu wa Serikali kuhusu hifadhi ya chakula. Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa zinanunua chakula cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa chakula hicho kiingie sokoni na hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama za chakula.

“Rais wetu kawaambia wananchi wa Kagera kwamba Serikali haina shamba hivyo hakuna chakula cha njaa. Hii kauli si ya uongozi. Ni kauli ya kuficha uamuzi wa Serikali uliotusababisha kukosa akiba ya chakula,” alisema.

Zitto alisema Ghala la Taifa la Chakula (NFRA) lina tani 90,000 tu za chakula wakati kwa kipindi kama hiki mwaka juzi lilikuwa na tani 450,000.

Kwa mantiki hiyo, alisema chakula kilichopo kwa sasa ndani ya ghala hilo kinatosha kwa wiki moja kwa mujibu wa takwimu katika taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mapitio ya uchumi ya Novemba, mwaka jana.

“Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba, alijibu hoja hizi kwa wepesi kabisa na kusema kwamba Tanzania ina chakula cha kutosha. Alipoulizwa ataje kiasi kilichopo NFRA, alijibu kwa sababu za kiusalama hawezi kutaja,” alisema.

Zitto alikwenda mbali kwa kumpongeza  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa kuamua yeye mwenyewe kutembelea NFRA na kujionea hali halisi.

Alisema alichokifanya Majaliwa ndio uongozi na si viongozi kukanusha habari ambazo ni za kweli na zilishathibitishwa na taasisi za Serikali kama BoT na alimtaka kuwachukulia hatua viongozi wa Serikali wanaoficha ukweli kuhusu baa la njaa.

“Waziri wa Kilimo anasema kama wananchi wanaona ugali ni ghali wale wali. Anasema kuna mchele mwingi nchini, lakini umeshikwa na watu binafsi. Waziri anataka kuwaambia Watanzania kuwa hivi sasa Serikali inategemea chakula cha watu binafsi ambao haijui idadi ya tani zilizopo kushughulika na suala la njaa.

“Hii ni ajabu kubwa sana, nchini Ufaransa alitokea mke wa mfalme mmoja. Wananchi walikuwa wanalalamika kuwa hakuna mikate. Malkia yule akiitwa Marie Antonnoite, alimwambia mumewe, hawa watu wako kama hawana mikate si wale keki? Hii ndio hali ya sasa nchini. Waziri anasema kama sembe imekuwa ghali, wananchi wale wali. Anasahau kuwa hata mchele umepanda bei. Maharage yamepanda bei na mafuta ya kupikia yamepanda bei,” alisema.

 Kauli ya Majaliwa

Katikati ya wiki hii, Majaliwa, akiwa mkoani Ruvuma alitoa agizo la kusisitiza kutunza chakula kwa kusema akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.

Alitoa agizo hilo baada ya kukagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na NFRA Kanda ya Songea.

Alisema kawaida mwezi huu mvua za kutosha huwa zinanyesha na huwa kuna baridi lakini mwaka huu imekuwa tofauti kwa sababu kunashuhudia kuwapo joto kali.

“Kama mvua haijanyesha hadi leo ni lazima tuchukue tahadhari, hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani,” alisema.

Majaliwa aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ahsante mheshimiwa zitto kabwe kwa taarifa yako kwa umma Tanzania inawategemea wapinzani mtoe uozo ni mipango batili ya serikali

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles