23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO AACHIWA KWA DHAMANA YA MIL 50

NA RAMADHAN LIBENANGA -MOROGORO

JESHI  la polisi Mkoani Morogoro jana lilimuachia  kwa dhamana ya bondi  yenye thamani  Sh. milioni 50, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, baada ya kulala rumande siku moja katika Kituo cha Polisi Morogoro.

Taarifa iliyotolewa jana na  na Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamisi, ilieleza kuwa, Zitto ambaye  alikamatwa juzi katika  tarafa ya Mgeta wilayani Mvomero mkoani Morogoro kwa tuhuma ya kufanya mkutano bila kibali aliachiwa kwa  kudhaminiwa na Wakili wake Emmanuel Mvula baada ya kuandika maelezo.

Kabla ya kupatiwa dhamana hiyo jana  taarifa ya  awali iliyotumwa juzi usiku na Khamisi ilieleza kuwa  polisi walikataa kumpatia dhamana Zitto pamoja na kuandika maelezo akiwa na wakili wake kuanzia saa 4:42  hadi 5:40 usiku.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi Ulrich Matei alisema, Zitto alikamatwa  juzi akiwa katika  tarafa ya Mgeta wilayani Mvomero mkoani Morogoro akituhumiwa kufanya mkutano wa hadhara pasipo kibali jambo ambalo ni kinyume na sheria kwa mujibu kifungu cha sheria  namba 74/75.

Kwa mujibu wa Kamanda Matei alisema Zitto alifika katika eneo hilo kwa lengo la kufanya kikao cha ndani na wanachama na ACT wazalendo wilayani humo.

“Mara baada ya watu kuongezeka waliamua kutoka nje na kufanya mkutano wa hadhara kinyume na sheria kifungu cha sheria namba 74/75,”alisema  Kamanda Matei.

Matei alisema pamoja na kupewa dhamana hiyo, Zitto anatakiwa kurudi kituoni hapo Machi 3 mwaka huu.

Akizungumza nje ya kituo cha polisi mara baada ya kuachiwa kwa dhamana, Zitto alisema matatizo ya viongozi wa kisiasa kukamatwa wakiwa katika mikutano na maandano yameanza kipindi cha utawala huu.

“Haya matatizo yameanza katika utawala huu, huko nyuma tulikuwa tunafanya mikutano,maandamano bila shida yeyote utawala huu ndiyo ambao hautaki watu wazungumze na watu wengine,hautaki viongozi  waonane na wananchi wanataka tuwasikie wao tu kupitia TV zao na magazeti yao,”alisema Zitto.

Alisema wanasiasa wana wajibu wa kupambana kuhakikisha hali iliyopo sasa  kwa wananchi kuminywa uhuru wa kukutana inabadilika.

“Lengo ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa  ya kidemokrasi na wananchi wanapata haki zao za msingi bila bugudha zozote,moja ya haki za msingi  ni haki ya kukutana ni haki ya kikatiba  ambayo hamna mtu mwenye mamlaka ya kutunyang’anya,”alisema Zitto.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles