ZINAHITAJIKA HATUA MADHUBUTI KULIOKOA ZAO LA PAMBA

0
509

PAMBA ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara nchini.  Ni kati ya mazao ambayo yamekuwa yakiliingizia taifa fedha nyingi za kigeni tangu uhuru.

Lakini katika miaka mingi sasa kilimo cha zao hilo kimekumbwa na msukosuko kutokana na utaratibu mbovu na ukiukwaji wa mfumo mzima  wa kilimo hicho ambao umekuwa ukifanywa na wadau kwa ujumla.

Msukosuko huo umeikumba sekta nzima ya pamba kuanzia wakati wa kulima, upaliliaji, matumizi ya mbolea, mbegu na masoko.

Bahati mbaya ni kwamba kilimo hicho cha pamba kimekuwa kikivurugwa na pande zote zinazohusika kuanzia kwa wakulima wenyewe, makampuni yanayonunua pamba na taasisi inayosimamia zao hilo, kwa maana ya Bodi ya Pamba Tanzania.

Kwa mfano makampuni yanayonunua pamba yamekuwa yakijihusisha katika udanganyifu mkubwa pamoja na kukiuka taratibu za ununuzi wa zao hilo.

Pamoja na mambo mengine, makampuni hayo yamekuwa yakifanya udanganyifu huo kupitia mizani zake kwa kuzifanya zisisome uzito halisi wa pamba inayonunuliwa na hivyo kuwaibia wakulima.

Umuhimu wa pamba katika taifa ni suala lisilohitaji   mjadala, ndiyo sababu  tunaunga mkono  hatua iliyochukuliwa na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuhakiki mizani za makampuni ya kununua pamba katika Mkoa wa Simiyu, lengo likiwa ni kuhakikisha wakulima hawaibiwi.

Meneja wa WMA katika mkoa huo, Augustine Maziku, alikaririwa akisema kuwa mizani 1,500 za makampuni hayo zimekwisha kukaguliwa.

Matarajio  ni kwamba hatua hiyo itatekelezwa hata katika mikoa mingine inayolima zao hilo, hususan ya Kanda ya Ziwa na mingine.

Jambo jingine ambalo limekuwa likichangia kudidimiza kilimo cha pamba ni baadhi ya makampuni ya mbegu ambayo yamekuwa yakiuwauzia wakulima mbegu ambazo siyo bora na ambazo wakati mwingine hazioti.

Ni tatizo ambalo linapaswa kutafutiwa ufumbuzi madhubuti na wa kudumu kwa kuyachukulia hatua kali makampuni ya aina hiyo, ikiwamo kuyang’anya leseni.

Kikwazo kingine ambacho nacho kimekuwa kikichangia kwa kiasi chake kuwakatisha tamaa wakulima ni bei ya kuuzia pamba yao.

Kwa miaka nenda rudi, wakulima wamekuwa wakilalamika kuwa bei ndogo mno ikizingatiwa gharama ambazo wamekuwa wakizitumia kuanzia kulima, kupalilia, kunyunyizia dawa hadi kuvuna na kuuza.

Hilo ni suala ambalo hadi sasa halijapata ufumbuzi wa kudumu kwa sababu ya mvutano ambao umekuwapo kati ya Bodi ya Pamba kwa maana ya serikali na makampuni yanayonunua pamba.

Mara nyingi makampuni hayo yamekuwa yakitaka kununua pamba kutoka kwa mkulima kwa bei ndogo huku yakitoa sababu zisizokuwa na msingi kuwa yakinunua kwa bei kubwa yanapata hasara.

Lakini pengine suala jingine ambalo linasikitisha ni ‘hujuma’ ambayo hufanywa na wakulima wenyewe.  Baadhi ya wakulima hao, kwa kutaka kupata fedha nyingi, wamekuwa wakiimwagia maji pamba yao wanapokwenda kuiuza ili iwe na uzito zaidi.  Wakati mwingine wamekuwa wakiweka mawe madogo iweze kuwa na uzito zaidi.

Pamba kama hiyo ikisafirishwa nje imekuwa ikinunuliwa kwa bei ndogo sababu ni chafu.

Kama tulivyosema awali, haya ni matatizo ambayo yamesababisha kilimo cha pamba kushuka kwa kiwango kikubwa, mambo ambayo yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi mapema.

Matarajio yetu ni kwamba pande zote zinazohusika zinapaswa kushirikiana na kuchukua hatua madhubuti kuliwezesha zao hilo kushika nafasi yake katika uchumi na maendeleo ya taifa hili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here