Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM
JESHI la Zimamoto na Uokoaji nchini linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa yakiwamo magari, vituo vya kutolea huduma pamoja na wafanyakazi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamishna Generali wa Jeshi hilo, Thobias Andengenye, alisema lengo ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya shughuli zinazofanywa na Jeshi hilo.
Mbali na hilo, Andengenye alisema wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu, uhaba wa wafanyakazi na uelewa mdogo kwa wananchi kuhusiana na shughuli za uokoaji.
“Changamoto hizi zinasababisha kuchelewa kwa huduma inapotokea ajali ya moto katika eneo la tukio, suala ambalo limekuwa linapigiwa kelele na wananchi,” alisema.
Aidha, katika changamoto hizo, alisema Watanzania hawana utamaduni wa kupisha magari ya uokoaji pale yanapokuwa yanatakiwa kuwahi kuzima moto.
“Tunaomba kampuni za simu kuweka utaratibu maalumu wa namba kama vile 112 na 114 ili kuepusha watu wanaotaka kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” alisema.
Kamishna Generali Andengenye alisema kwa mwaka 2016/17, walifanikiwa kukagua maeneo 25,418 yenye vifaa vya tahadhari vya kuzimia moto na lengo ni kufikia maeneo yote.
Alisema hivi karibuni wameanzisha vituo vya zimamoto na uokoaji katika maeneo ya Ubungo na Kigamboni na vipo katika hatua ya kumalizika ujenzi wake.
Aliwashauri wananchi kupeleka ramani za nyumba kabla ya kujenga nyumba zao ili watakapojenga wazingatie kuweka maeneo ya tahadhari mbalimbali.