Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
SERIKALI imetenga Sh milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa itasaidia kupunguza upungufu wa sare za askari wa jeshi hilo katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye alisema kwa mwaka huu mpya wa fedha, Serikali imeendelea kutatua changamoto za uhaba wa vitendea kazi ndani ya jeshi hilo.
Changamoto hizo ni kama vile magari na madawa ya kuzima moto ambako zimetengwa Sh bilioni tatu mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kununua magari, ongezeko ambalo ni maradufu ya kiasi kilichotolewa mwaka wa fedha uliopita.
Alisema katika mwaka wa fedha uliopita wa 2016/2017 Serikali ilitenga Sh bilioni 1.5 kwa ajili ununuzi wa magari ya kuzima moto.
Alisema jitihada hizo za Serikali zinalenga kuondoa changamoto ya uhaba wa vitendea kazi na hivyo kurahisisha utendaji kazi wa jeshi hilo.
Kamishna Andengenye alisema mbali na ununuzi wa magari Serikali pia imeweka juhudi katika suala zima la ununuzi wa madawa ya kuzima moto ambako Sh milioni 500 zimetengwa katika katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi wa madawa ya kuzima moto.