30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

ZIJUE SABABU ZA WATU KUDANGANYA

Na Christian Bwaya,

FIKIRIA unavyojisikia pale mtu wa karibu unayemwamini anapokudanganya. Huwezi kufurahia. Uongo, kwa kawaida, unakatisha tama na unaumiza. Wakati mwingine unatafsiriwa kama usaliti. Mtu asiyesema ukweli anasaliti imani waliyonayo watu kwake. Uongo haupendezi.

Ingawa wengi wetu hatupendi kudanganywa, kuna mazingira fulani fulani nasi hujikuta tumedanganya. Kwa mfano, rafiki yako anakuuliza uliko au unakokwenda, unaamua kumtajia kwingine. Unaweza kufikiri ni jambo dogo lakini tabia hii inatia doa uhusiano wako na watu.

Kwanini watu hudanganya?

Kisaikolojia zipo sababu kuu mbili zinazofanya watu wadanganye. Kwanza, watu hutumia uongo kama njia ya kurekebisha mambo pale wanapokabiliwa na hatari ya kupoteza heshima yao. Kwa mfano, unaposhindwa kufanya jambo unalojua linatarajiwa au unapofanya jambo unalojua halikutarajiwa, unajisikia vibaya. Ndani yako unasikia hatia ya kuwa mkosaji. Unakuwa na wasiwasi kuwa kosa ulilofanya linaweza kuharibu uhusiano wako na yule uliyemkosea. Uongo, kwenye mazingira kama haya, unakuwa ni chaguo baya lakini lenye unafuu kwa lengo la kulinda uhusiano na mtu aliyekosewa.

Sababu ya pili ni kudanganya kwa lengo la kusababisha maumivu kwa mtu aliyekuumiza. Hapa mwongo hadanganyi kulinda uhusiano wake na yule anayemdanganya bali kulipiza kisasi kwa maumivu anayoamini amesababishiwa na huyo anayemdanganya. Kwa mfano, unapomfanya mtu ajisikie umemvunjia heshima, labda kwa kumdanganya, ni rahisi na yeye kutafuta namna ya kukuvunjia heshima kwa kukudanganya.

Ikiwa unapenda watu wanaokuzunguka wakuambie ukweli, siri ni kufanya mambo matatu makubwa.

Usiweke mazingira ya kudanganywa 

Si kila taarifa unayoihitaji kwa mtu ni ya lazima. Pia, si kila taarifa unayoihitaji kwa mtu inapatikana. Kuna maswali unaweza kumwuliza mtu yakamshawishi kukudanganya. Kwa mfano, maswali ambayo majibu yake yanaweza kuibua utata, yakamfanya mtu asijikie vibaya, yakamkumbusha uchungu aliowahi kukutana nao, ni kichocheo cha kudanganywa.

Kabla hujauliza kupata taarifa fulani kwa mtu, jiulize kama kufanya hivyo ni lazima. Ikiwa ni lazima kuulizia suala hilo, angalia namna ya kuuliza ili majibu ya swali yasimfanye mtu akajisikia kudhalilika.

Kwa mfano, kama una mpenzi wako, unapohoji masuala ya wapenzi wake wa zamani unaowafahamu, ni wazi unachokoza mzinga wa nyuki bila sababu. Je, ni lazima ujue historia isiyokusaidia? Ikiwa ni lazima kuijua, basi epuka kuonekana unatafuta habari zinazomdhalilisha mwenzako. Hilo la kwanza.

 Angalia unavyoupokea ukweli

Labda ni namna unavyouchukulia ukweli usioupenda. Unadanganywa kwa sababu pengine anayekudanganya anajua ukweli haulindi uhusiano wenu. Unapoambiwa ukweli unajenga mazingira ya kumfanya aliyesema ukweli huo ajilaumu kwa nini alisema alichokisema. Ukweli unageuka kuwa ugomvi usiotarajiwa, unakasirika, unahukumu na kulalamika kwa sababu tu umepewa taarifa usizozitarajia.

Unafanyaje unapoambiwa ukweli usioutaka? Unakasirika au unalaumu? Haipaswi kuwa hivyo. Jenga tabia ya kuupokea ukweli bila ugomvi hata kama anayekwambia anakiri kosa. Shughulikia kosa kwa namna chanya ukijua hata wewe unaweza kukosea. Unapofanya hivyo, unamfanya mwenzako siku nyingine asisite kukuambia jambo lolote kwa sababu anajua ukweli hautamgharimu.

 Onesha mfano

Wakati mwingine unadanganywa kwa sababu hicho ndicho unachokifanya wewe. Huwezi kutegemea watu wanaoathirika na uongo wako wakuambie ukweli. Unavuna kile ulichokipanda. Unahitaji kufanya kinyume. Onesha mfano kwa watu kwa kuwaambia ukweli. Sema kweli, na wewe utaambiwa ukweli.

Lakini pia, kama tulivyodokeza awali, wakati mwingine watu huweza kukudanganya kwa sababu wanalipiza kisasi kwa mambo uliyowafanyia. Kwa mfano kama huna tabia ya kuwaheshimu watu na wao watatumia uongo kama namna ya kukuadhibu.

Jenga tabia ya kuwaheshimu watu unaofanya nao kazi au unaoishi nao. Heshima itawasukuma kukuheshimu. Ukweli ni namna moja wapo ya kukuheshimu.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles