KOCHA wa Real Madrid, Zinedine Zidane, amesema hawezi kumuuza mshambuliaji wake, Cristiano Ronaldo kwa kuwa mchango wake ni mkubwa.
Baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo kupitia mitandao ya kijamii walidai mchezaji huyo auzwe kutokana na uwezo wake kuonekana kushuka katika baadhi ya michezo.
Ila Ronaldo aliwajibu mashabiki hao kwa vitendo ambapo alifanikiwa kutupia mabao manne katika ushindi wa 7-1 dhidi ya Celta Vigo katika michuano ya Ligi Kuu nchini Hispania na kumfanya Zidane akane kumuuza.
“Kuna shabiki yeyote ambaye anataka Ronaldo auzwe? Sawa lakini niwaweke wazi kwamba kitu hicho kwa upande wangu hakiwezekani nikiwa kama kocha.
“Kama wapo ambao wanataka Ronaldo aondoke basi na mimi nipo tayari kuondoka, timu ikiwa inafanya vibaya hasiangaliwe mchezaji mmoja na hata ikishinda wanatakiwa wachezaji wote waangaliwe.
“Kikubwa ni kwamba, mashabiki wanatakiwa kuwaunga mkono wachezaji wao kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho,” alisema Zidane.
Klabu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi huku ikiachwa pointi 12 na wapinzani wao ambao wanaongoza ligi hiyo Barcelona yenye pointi 72, huku Atletico Madrid ikiwa na pointi 64 ikishika nafasi ya pili.