ZIARA YA TTB ISRAEL YALETA MAFANIKIO

0
646
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi. Devota Mdachi akitoa mada katika mkutano nchini Israel alipofanya ziara ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na fursa za biashara kupitia sekta hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi. Devota Mdachi akitoa mada katika mkutano nchini Israel alipofanya ziara ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na fursa za biashara kupitia sekta hiyo.

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BODI ya Utalii Israel imeahidi kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kutangaza vivutio vilivyopo na kukuza sekta ya utalii nchini.

Akizungumza jana Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi,  aliyeongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki, kuitembelea Israeli kwa siku tatu mapema mwezi huu, alisema imeleta mafanikio makubwa katika sekta ya utalii nchini.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni  kukutana na wadau wa sekta ya utalii wakiwamo mawakala wa utalii na sekta ya malazi.

“Israel imeonesha shauku kubwa ya kushirikiana na sisi katika kuutangaza utalii wa Tanzania. Mwaka jana tulipata watalii  22,000 kutoka nchini humo ambapo wameahidi mwaka huu watakuja watalii wengi zaidi.

“Vilevile kupitia vyombo vyao vya habari tumeeleza namna vivutio vyetu vilivyo na mwonekano wa kipekee duniani, tumepokea maombi mengi ya kuja kutembelea fukwe na hifadhi za wanyamapori,” alisema.

Alieleza kuwa hifadhi zilizotajwa sana ni Katavi, Mahale, Ngorongoro na Zanzibar.

“Tunafahamu Waisraeli wanapenda kuangalia wanyamapori. Nilipokuwa nikiwatajia wanayama tulio nao walionesha kufurahi hasa nilipowaeleza kuwa faru Fausta (55) mwenye umri mkubwa kuliko wote barani Afrika yupo katika ardhi ya Tanzania walionyesha kuvutiwa zaidi,” alisema

Akizungumza katika mkutano huo wa pamoja, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Nzuki  alisema wadau wa utalii nchini Israel katika Mji waTel Aviv.

“Tanzania kuna fursa nyingi katika uwekezaji,  upande wa hoteli za kitalii.  Ikiwa una kampuni ya kitalii pamoja nyumba ya wageni ya kisasa unajiwekea uhakika wa kupata wageni wengi.

“Ukiwa tayari unaweza kuja na kufuata utaratibu wa kisheria katika mamlaka husika utapewa maelekezo. Tunawakaribisha kuwekeza katika utalii,” alisema.

Miongoni mwa wawekezaji wanaofanya shughuli za kitalii nchini , Alon Hovev anayemiliki kampuni ya utalii ya Sima Safari , ameuambia mkutano huo kuwa sababu zilizomfanya kuwekeza Tanzania ni hali ya hewa na watu wake.

Mwaka jana sekta ya utalii iliingiza Dola za Kimarekani bilioni 2 ikiwa ni sawa na Sh Trilioni 4, mwaka 2014 iliingiza Dola bilioni 1.9.

Kiwango hicho cha mapato kiliifanya sekta ya utalii kuchangia asilimia 17.5 ya pato la taifa katika bajeti ya mwaka 2016/17 pamoja na kuingiza asilimia 25 ya fedha za kigeni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here