Ziara ya Majaliwa yaacha vumbi Morogoro

0
590

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumwonya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mussa Mnyeti kwa kugombania miradi ya maendeleo, Rais Dk. John Magufuli amewatumbua watendaji hao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, nafasi zilizoachwa wazi na wawili hao zitajazwa baadaye.

Majaliwa ambaye yuko katika ziara ya siku tano mkoani Morogoro, juzi akiwa Malinyi aliwaonya viongozi hao kuacha kugombania miradi na mingine wakiichakachua.

Alitoa onyo hilo wakati akizungumza na watumishi wa wilaya hiyo pamoja na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Toboa mkoani Morogoro.

Kutokana na hilo, Majaliwa aliagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Lauren Ndumbaro kuchunguza weledi wa utendaji kazi wao.

Mapema wiki hii, Majaliwa akiwa katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara aliwasimamisha watumishi wengine saba kwa tuhuma za ufisadi.  

Mbali na hilo, juzi akiwa Ulanga pia aliwasimamisha kazi watumishi nane huku akiagiza wafikishe mahakamani kujibu tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh bilioni 3 za mapato ya ndani.

“Nawasihi nyote muache kufanya kazi kwa mazoea. Mbadilike na kuenenda sawa na matakwa na maelekezo ya Serikali ya awamu ya tano na anayejiona hatoshi ajiondoe,” alisema.

Aliwataja watumishi hao nane kuwa ni Yusuph Semguruka aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo ambaye kwa sasa amehamishiwa Tamisemi, Rajab Siriwa (mweka hazina), Stanley Nyange, John Mwenyembole, Isack Mwansokope, Said Majaliwa, Charles Steven na Hezron Lopa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here