Ziara ya JPM yavunja Bodi Uhuru

0
514
Rais John Magufuli
Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika Kampuni ya Uhuru inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Bodi ya kampuni hiyo imejiuzulu.

Juzi Rais Magufuli alifanya ziara katika kampuni hiyo kama Mwenyekiti wa CCM, pamoja na mambo mengine alisikiliza matatizo waliyonayo wafanyakazi wa kampuni hiyo, ambapo iligundulika kuwa walikuwa hawajalipwa mishahara kwa muda wa miezi saba.

Mbali na hilo, Rais Magufuli aliahidi kuzikata fedha wizara zote zinazodaiwa na kampuni hiyo ili ziweze kulipa deni la Sh bilioni 1.6 ambalo limelimbikizwa kwa muda mrefu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka alisema Bodi ya Uhuru Media Group inayosimamia vyombo vya habari vya chama hicho tawala, imejiuzulu kupitia barua ya Mwenyekiti wa bodi hiyo, Adam Kimbisa.

“Bodi ya Uhuru Media Group inayosimamia vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambavyo ni Uhuru Publications Limited (UPL) wachapishaji wa Gazeti la Uhuru, Mzalendo na Burudani pamoja na Peoples’ Media Communication Limited (PMCL) inayoendesha kituo cha redio Uhuru imejiuzulu kupitia barua ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Adam Kimbisa,”alisema Sendeka.

Aidha alisema Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais John Magufuli amepokea barua ya kujiuzulu kwa bodi hiyo huku nakala nyingine ikienda kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here