26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

ZAWADI YA MAKONDA KWA MWENYEKITI WA MTAA YAPINGWA

makonda

Na TUNU NASSOR

-DAR ES SALAAM

JINAMIZI la uchaguzi mkuu wa mwaka jana limeendelea kuukumba Mtaa wa Mivinjeni, Kata ya Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam baada ya baadhi ya wajumbe wa Serikali ya mtaa huo kupinga zawadi ya pikipiki iliyotolewa kwa Mwenyekiti wao, Barua Mwakilanga.

Akiwa katika ziara aliyoipa jina la ‘Dar mpya’, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alimtangaza Mwakilanga kuwa ndiye mwenyekiti bora wa mtaa bora kuliko wote jijini, na kuwataka wengine kuiga mfano kwake, huku akimzawadia pikipiki.

Wajumbe hao wamedai kuwa Mwakilanga hakustahili heshima hiyo kutokana na mtaa wao kuwa na changamoto kadhaa ambazo bado hazijatolewa ufumbuzi.

Mmoja wa wajumbe hao, Mtumwa Abdallah, alisema Makonda hakuwatendea haki katika kutekeleza uamuzi wake huo, alipaswa kuwasikiliza juu ya utendaji wa mwenyekiti huyo.

Alisema zawadi hiyo itamfanya mwenyekiti huyo kuwa na kiburi, huku akiendeleza hujuma kwa wananchi wake, ambao anadai huwa hawasikilizi na kuwaitia polisi kila wanapomwita.

“Mwenyekiti huyu amechimba visima 13 bila kufuata utaratibu, kapokea fedha za miradi na kuzielekeza katika matumizi yasiyosahihi na upotevu wa vyerehani 35 vya mtaa,” alidai Mtumwa.

Akijibu malalamiko na madai hayo, Mwakilanga alisema madai hayo yanatokana na mwendelezo wa makundi ya uchaguzi wa mwaka jana.

Alisema tangu aingie madarakani ametatua kero nyingi za wananchi, ikiwamo upungufu wa umeme na ajira za vijana.

“Nimesimamia uwekwaji wa ‘transformer’ tatu kupunguza kero ya umeme ambayo ilikuwa ikiwakabili mtaani hapa, pia nimenunua vyerehani 175 ambavyo vinatumika kutoa mafunzo kwa vijana wetu,” alisema Mwakilanga.

Alisema mjumbe aliyetoa madai hayo kwa sasa amesimamishwa kazi kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha. Kwamba alikubali kwa maandishi tuhuma hizo na kutakiwa kuzirejesha ndipo arudi kazini.

“Mtumwa alitumia fedha za mtaa katika kubeti na kuvuta kilevi aina ya shisha, na ni miongoni mwa kundi lililojipanga kurudisha nyuma maendeleo ya mtaa wetu,” alidai.

Aliongeza kuwa kama kundi hilo litaendelea litakwamisha juhudi za wahisani wanaotaka kusaidia miradi ya mtaa huo kama ujenzi wa kituo cha polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles