24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

ZATAKIWA BENKI ZA NYUMBA, MIKOPO INAYOTOLEWA HAITOSHI

Na BAKARI KIMWANGA-DAR ES SALAAM


MWANZONI mwa miaka ya 1960, mikopo ya nyumba ilikuwa ikitolewa taasisi ya ‘First Permanent Building’ Society iliyokuwa imesajiliwa nchini
Zambia, wakati huo ikijulikana kama nchi ya Rhodesia Kaskazini, lakini pia ilikuwa na matawi katika nchi za Afrika Mashariki.

Mwaka 1963, muundo wa matawi ya kampuni hiyo yaliyokuwa Afrika Mashariki, ulibadilishwa na kuundwa kwa First Permanent East Africa Ltd. Wawekezaji kwenye kampuni hiyo walikuwa ni Serikali za nchi za Afrika Mashariki pamoja na Commonwealth Development Corporation (CDC).

Mwaka 1968, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Commonwealth Development Corporation, iliunda Permanent Housing Finance Company (PHFC) Ltd, ambayo ilirithi majukumu ya First Permanent East Africa
Ltd.

Hata hivyo, mwaka 1972, Serikali ya Tanzania ilitaifisha Permanent Housing Finance Company (PHFC) Ltd, baada ya kuonekana kama kampuni hiyo ilikuwa ikilinda masilahi ya wageni zaidi, ambapo kufuatia utaifishaji huo, Serikali ilianzisha Benki ya Nyumba Tanzania (Tanzania Housing Bank) au THB.

Wawekezaji katika Benki ya Nyumba Tanzania walikuwa ni Serikali ya Tanzania, asilimia 46.5; Shirika la Bima la Taifa-asilimia 30.2 na National Provident Fund-asilimia 23.3.

Mnamo mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tanzania ilianza mchakato wa maboresho katika sekta ya fedha yaliyojulikana kama Financial Sector Liberalization and Reform. Mchakato huu ulitokana na ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, iliyojulikana kama Tume ya Nyirabu (Nyirabu Commission). Charles Nyirabu ndio alikuwa Gavana wa Benki Kuu wakati huo.

Baraka Munisi ni Mtaalamu wa Masuala ya Mikopo ya Nyumba kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anasema kutokana na hali hiyo, Tume ilitathmini maendeleo katika sekta ya fedha na kuainisha marekebisho kadhaa muhimu katika sekta hiyo ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika programu ya kurekebisha uchumi na moja ya mapendekezo ya Tume ya Nyirabu ilikuwa ni kuwa Serikali itunge sera/sheria itakayowezesha upatikanaji wa mikopo ya nyumba.

Mapendekezo ya Tume ya Nyirabu yalifanyiwa kazi chini ya mradi wa Financial Sector Development Project (FSDP), uliofadhiliwa na Serikali ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (International Development Association (IDA).

Baadhi ya matokeo ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Nyirabu ni pamoja na kutungwa kwa  Sheria ya
Mikopo ya Nyumba (The Mortgage Finance (Special Provisions Act) iliyotungwa mnamo mwaka 2008.

 

Mradi wa mikopo ya nyumba

Anasema jitihada hii ya Serikali ya kuhakikisha maboresho zaidi katika sekta ya mikopo ya nyumba ilifuatiwa na uanzishwaji wa mradi wa Housing Finance mnamo Machi 2010, mradi huo unaotokana na mkopo wa
takribani Dola za Marekani milioni 100 ambao Serikali iliupata kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo (IDA), taasisi ya Benki ya Dunia itoayo mikopo ya muda mrefu kwa riba nafuu  kwa nchi na kukasimu uendeshaji na usimamizi wake kwa Benki Kuu ya Tanzania.

“Mradi huu ni mwendelezo wa jitihada za kuendeleza upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu (access to long-term finance) ambazo zilikuwa zinasimamiwa na Benki Kuu chini ya programu ya maboresho za sekta ya
fedha (Financial Sector Reform Program). Mradi wa HFP unategemea kumalizika mnamo Machi 31, mwaka huu.

“Lengo kubwa la mradi huu ni kuendeleza sekta ya mikopo ya nyumba kwa kuweka mazingira ya upatikanaji wa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa mabenki na taasisi za fedha zinazohusika na utoaji wa mikopo ya nyumba kwa wananchi.

Hii inatokana na ukweli kwamba tangu kufungwa kwa benki ya nyumba (THB) mwaka 1995, mabenki na taasisi nyingi za fedha zimekuwa haziwezi kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wananchi kwa ajili ya ujenzi
wa nyumba kutokana na kukosa vyanzo vya fedha ambavyo ni vya muda mrefu (long-term financing),” anasema Munisi.

Anasema mabenki na taasisi hizo hutegemea zaidi amana za wananchi ambazo ni za muda mfupi katika kutoa mikopo na hivyo haziwezi kutoa mikopo ya muda mrefu kwani kwa kufanya hivyo zitaingia katika
changamoto ya ukwasi. Mradi huu unajihusisha zaidi na upatikanaji wa mikopo na si maendeleo ya nyumba na miundombinu ya makazi.

Mradi wa HFP

Akizungumzia mradi huo, Munisi anasema umegawanyika katika sehemu kubwa tatu  kama ifuatavyo;
Sehemu ya kwanza ni ile inayohusu uundwaji wa taasisi itakayotoa mikopo ya muda mrefu kwa mabenki na taasisi za fedha. Chini ya sehemu hii, taasisi ijulikanayo kama Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC) Limited, ilianzishwa mnamo mwaka 2011 kama kampuni binafsi inayomilikiwa na mabenki na taasisi za fedha.

Undwaji wa taasisi hii ulitokana na stadi mbalimbali zilizofanyika hususani katika nchi za Nigeria na Misri. TMRC hukopeshwa fedha kutoka kwenye mradi kwa kipindi fulani na kwa riba ya asilimia 10 kwa ajili ya kuzikopesha benki na taasisi za fedha ambazo ni wanachama.

“TMRC huweka dhamana (Collateral) kwa mikopo yote inayopokea kutoka kwenye mradi na kukopesha benki wanachama huku ikiwa inawajibika kwa majanga yote (risk) yanayoweza kutokana na hiyo mikopo.
“Katika azma nzima ya kuendeleza sekta ya mikopo ya nyumba na kuhakikisha unafuu wa mikopo hii kwa mabenki na taasisi za fedha wanachama, TMRC haipaswi kutoza riba inayozidi asilimia 1.5 juu ya
ile riba wanayotozwa wanapopewa mkopo toka kwenye mradi.

“Sehemu ya pili inalenga kuendeleza sekta ya mikopo kwa taasisi za fedha kwa ajili ya kukopesha wananchi wenye kipato cha chini mikopo ya ujenzi au uboreshaji wa nyumba yenye masharti nafuu (housing microfinance) na ya muda mrefu zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba wananchi wenye kipato cha chini ni vigumu sana kwao kuweza kupata mikopo ya kawaida ya nyumba (traditional mortgages) kutokana na kutokuwa na dhamana (collateral) na kipato rasmi.

“Chini ya sehemu hii, mnamo Aprili 2014, Serikali ilianzisha mfuko wa kukopesha taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba kwa wananchi walioko katika kundi hili unaojulikana kama Housing Micro Finance Fund
(HMFF) kwa kutoa waraka maalumu (The Public Finance Housing Micro Finance Fund Establishment) Order, 2014),” anasema.

Mtaalamu huyo wa mikopo ya nyumba anasema Serikali ilikasimu  usimamizi na uendeshaji wa mfuko huu kwa Benki Kuu ya Tanzania mnamo Mei, 2014 kwa njia ya mkataba ambapo mfuko huo ulitengewa jumla ya Dola
za Marekani milioni 18.0  kama  mtaji mbegu kwa ajili ya kuzikopesha taasisi za fedha zinazohusika.

Mafanikio
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17, mkazo mkubwa umewekwa katika kumalizia uratibu mradi wa Housing Finance Project ulioanza mwaka 2010 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu (2018). Mafanikio yanayotokana na uratibu wa mradi huu ni pamoja na haya yafuatayo:-

“Kuanzishwa kwa taasisi ijulikanayo kama Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC) kwa ajili ya kuzikopesha benki za biashara mikopo ya muda mrefu na hivyo kuziwezesha benki hizo kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wananchi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi. Kuanzishwa kwa TMRC kumeleta chachu kubwa katika upatikanaji wa mikopo ya nyumba na kuziwezesha benki nyingi zaidi za biashara kuanza kutoa mikopo hiyo.

“Jumla ya benki za biashara 30 zinatoa mikopo hii kwa sasa kutoka benki 3 mwaka 2011 kutokana na kuongezeka kwa ushindani riba za mikopo hii zimeshuka kutoka wastani wa asilimia 22 mwaka 2011 hadi asilimia
18 mwaka 2017.

“Muda wa mikopo hii umeongezeka kutoka miaka 5 hadi 10 mwaka 2011 na kufikia miaka 15 hadi 20 mwaka 2017, na kuifanya sasa mikopo ya ujenzi wa nyumba kuwa nafuu zaidi kwa mwananchi wa kawaida ambapo jumla ya wananchi 3,915 wamefaidika na mikopo kutoka katika benki za biashara kwa ajili ya ujenzi au ununuzi wa nyumba za makazi hadi kufikia Juni 2017,” anasema Munisi.

Anasema katika mikopo hiyo ya nyumba hadi sasa jumla za Sh bilioni 446  zimetolewa kwa ajili ya nyumba kwa wananchi ambazo ni sawa na asilimia  0.43 ya pato la Taifa.
Mafanikio mengine makubwa ni pamoja na kujengewa uwezo taasisi kadhaa  zinazojihusisha na ujenzi wa nyumba  kama vile National Housing  Corporation (NHC), National Housing, Building and Research Agency
(NHBRA), Watumishi Housing Company Limited na Benki Kuu ya Tanzania  kwa njia ya mafunzo na kupatiwa vifaa vya utendaji.

Kadhalika, programu ya kuelimisha umma wa Tanzania kuhusu dhana hii ya mikopo ya  nyumba za makazi (Mortgage Literacy Program) inaendelea na ilitarajiwa kumalizika Oktoba 2017.

Munisi anasema kupitia mradi wa HFP pia Serikali ilianzisha mfuko wa  mikopo ya nyumba za makazi kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha  chini (Housing Micro Finance Fund-HMFF) ili kuwawezesha wananchi hawa
ambao katika hali ya kawaida ni vigumu kupata mikopo hii kutoka katika  benki za biashara kutokana na kutokuwa na dhamana (collateral) na kipato cha kutosha.

Hadi Juni 2017 mabenki matatu yaani DCB Commercial Bank Plc, Yetu  Microfinance Bank Plc na EFC Tanzania M.F.B Limited ambazo zinahudumia  wananchi husika zimekwisha kopeshwa jumla ya shilingi za Tanzania
bilioni 9.0 na wananchi zaidi ya 300 wamekwisha faidika na mikopo  kutoka benki hizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles