20.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 28, 2022

ZANZIBAR KUKUZA UCHUMI KUPITIA TEKNOHAMA

 

Na MWANDISHI WETU, ZANZIBAR


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), inaelekeza nguvu zake katika kukuza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) ili kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki waliofanya ziara ya mafunzo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Teknolojia (Tehama) wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Mzee Suleiman Mndewa, alisema Zanzibar imejifunza mengi kutokana na jinsi Teknohama ilivyowezesha kukua kwa uchumi.

“Nchi za Asia zimeweza. Kwa sasa hakuna tofauti kati ya nchi nyingi za Asia na zile za Ulaya kuhusiana na maendeleo ya Teknohama.

“Vilevile Teknohama ni nguzo mojawapo zilizosaidia kupatikana kwa maendeleo ya kasi kwa nchi ya Mauritius. Hata sisi tunaweza kufikia viwango hivyo endapo tutawekeza kwa kasi zaidi katika miundombinu msingi ya kimkakati ya Teknohama,” alisema Dk. Mndewa.

Alisema sekta za viwanda, fedha, Teknohama na utalii ndizo zilizoivusha Mauritius kutoka kuwa nchi inayotegemea kilimo mara baada ya kujipatia uhuru wake kutoka kwa wakoloni mwaka 1968 mpaka kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia kiwango cha kuwa na uchumi wa kati wa juu hivi sasa.

kutokana na azma hiyo ya kukuza uchumi, Dk. Mndewa alisema SMZ imewekeza fedha za kutosha zilizotumika katika ujenzi wa mkongo wa taifa.

“Na sasa baada ya kukamilisha kazi ya ujenzi wa mkongo, tumeamua kusambaza huduma hii ili iweze kuwafikia na kutumika na wananchi wote badala ya sasa ambapo hutumika na ofisi za Serikali tu….Tunataka wananchi, wafanyabiashara na watoaji wa huduma za mtandao wa mawasiliano (intaneti) waje moja kwa moja na kujiunganisha na mtandano huu,” alisema.

Hii ina maana kampuni za mawasiliano hazitalazimika kujenga miundombinu yao, kwani zitaweza kuja na kuunganishiwa huduma hiyo na Serikali kutoka katika maeneo ya kuunganishia wateja.

“Ni matumaini yetu kuwa wafanyabiashara watakuja na kujipatia viwango vinavyoendana na mahitaji yao….Lengo letu ni kuona ujenzi wa miundombinu msingi ya Teknohama inachukuliwa kama jambo la msingi ambalo ni sawa kabisa na ujenzi wa barabara ili kila mwenye kupenda aweze kuitumia katika biashara yake,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,097FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles