27.1 C
Dar es Salaam
Friday, September 13, 2024

Contact us: [email protected]

Zaidi ya Washiriki 500 kushiriki Maadhimisho ya Wiki ya AZAKI 2024 jijini Arusha

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Zaidi ya washiriki 500 kutoka Asasi za Kiraia (AZAKI), sekta binafsi, serikali, na wadau mbalimbali wa maendeleo wanatarajiwa kushiriki maadhimisho ya Wiki ya AZAKI 2024, yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Septemba 9 hadi 13, mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge.

Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, amebainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu ya “Sauti, Dira na Thamani.

“Kauli mbiu hii inakusudia kuakisi matukio muhimu yanayoendelea nchini, yakiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, uchaguzi mkuu ujao, pamoja na uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

“Tupo katika kipindi muhimu sana kwenye demokrasia yetu kama nchi. Mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani tuna uchaguzi mkuu. Jambo la kipekee zaidi ni kwamba mwakani tunatarajia kuzindua Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, fursa adimu ambayo huja mara moja kwa muda mrefu,” alisema Rutenge.

Alisisitiza kuwa, kutokana na umuhimu wa fursa hii, ni lazima sauti za wananchi zisikike katika kuchangia maoni yao, kwani dira hiyo inapaswa kutokana na sauti, mawazo, na mitazamo ya wananchi.

Rutenge pia alieleza kuwa maadhimisho ya wiki hiyo yatakuwa na mijadala mbalimbali inayohusu shughuli za AZAKI nchini, maendeleo ya jamii, na ushirikiano baina ya Asasi za Kiraia, serikali, na sekta binafsi.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la CBM linalosaidia watu wenye ulemavu wa macho nchini, Nesia Mahenge, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya AZAKI 2024, alithibitisha kuwa maandalizi yamekamilika.

Mahenge aliwashukuru wadau wote waliodhamini na kuwezesha maadhimisho hayo, akiongeza kuwa wiki hiyo itawaleta pamoja makundi mbalimbali kama vijana, jamii, makundi maalum, na wadau watakaoshiriki katika mijadala ya mada zinazohusiana na kauli mbiu ya mwaka huu.

Hii ni mara ya sita kwa Wiki ya AZAKI kuadhimishwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles