27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Zaidi ya nusu ya madaktari, walimu nchini ni bomu

ummy

* Wengi wabainika hawana ujuzi wa kutibu, kufundisha

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

NI majanga katika sekta ya afya na elimu. Ndivyo unavyoweza kusema, kutokana na utafiti mpya kuonesha kuwa, madaktari na walimu wengi nchini hawana weledi na ujuzi katika kazi zao.

Mbali na upungufu huo pia mahudhurio yao katika vituo vyao vya kazi ni hafifu.

Utafiti huo kuhusu utoaji wa huduma za afya na elimu nchini (SDI) ulifanywa  na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini nchini (REPOA), kwa kushirikiana na Shirika la Utafiti wa Uchumi Afrika (AERC).

Ripoti hiyo imeeleza kuwa daktari mmoja kati ya watano ndiye mwenye uwezo wa kutoa matibabu sahihi ya magonjwa matano yanayoweza kutibiwa katika vituo vya afya na zahanati nchini.

Taarifa hizo zimekuja huku nchi ikikabiliwa na uhaba wa dawa muhimu hasa za maumivu (Panadol) pamoja na chanjo muhimu ikiwemo ya mbwa.

Mbali na ujuzi wa watoa huduma, utafiti huo ambao ulijikita katika huduma ya afya na elimu pia uliangazia upatikanaji wa rasilimali na jitihada za watoa huduma katika kutekeleza majukumu yao.

Akitoa ripoti hiyo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtafiti Mwandamizi wa REPOA, Dk. Lucas Katera alisema utafiti huo ulifanyika katika vituo 400 vya afya na shule za msingi 400 zenye sifa za kuwakilisha nchi nzima.

Alisema utafiti huo ulifanyika mwaka 2014 na ripoti yake ilizinduliwa rasmi Aprili 28, mwaka huu na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome.

Dk. Katera alisema magonjwa yaliyotumika kama kipimo kwa madaktari hao ni  Kifua Kikuu  (TB), Malaria, Limonia, Kisukari na Kuhara huku wataalamu waliofanyiwa utafiti wakiwa ni pamoja na madaktari, mauguzi na maofisa kliniki.

Alisema utafiti huo pia umeonesha tofauti iliyopo kati ya wataalamu wa afya wa mijini na vijijini ambapo kwa upande wa vijijini waliweza kutibu kwa usahihi asilimia 44 ya magonjwa hayo huku mjini ikiwa ni asilimia 70.

Katika uchambuzi huo wa ripoti, utafiti umebaini kuwa madaktari wengi wa mijini hawahudhurii kikamilifu katika vituo vyao vya kazi kwa asilimia 35 na vijijini ni asilimia 14 tu ambao hawakuwepo katika vituo vyao vya kazi.

Kuhusu upatikanaji wa rasilimali na miundombinu kwenye vituo vya afya na zahanati alisema asilimia 50 ya vituo hivyo havikuwa na huduma ya umeme na maji safi.

Dk. Katera aligusia upatikanaji wa chanjo zinazohifadhiwa kwenye majokofu ambapo alisema majokofu mawili kati ya matatu hayakuwa na viwango sahihi vya joto linalohitajika kwa uhifadhi.

“Hii ina maana kwamba pamoja na kuwepo kwa chanjo za kinga kwa ajili ya magonjwa mbalimbali kuna uwezekano mkubwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinaendelea kwa sababu chanjo wanazozipata hazina viwango vinavyotakiwa,” alisema Dk. Katera

Mbali na hili alisema kuwa asilimia 59 ya dawa muhimu kwa wajawazito hazikuwepo ambapo ni asilimia 8 tu ya vituo vilikuwa na dawa zote 14 muhimu hali ikiwa mbaya kwa vijijini kwa asilimia moja.

Hivi karibuni ilielezwa kuwa sekta ya afya imetetereka, kutokana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuwa na akiba ya makopo 173 ya vidonge vya Panadol kwa nchi nzima.

Mbali na hilo vifaa vya kujifungulia wanawake wajawazito navyo vimekosekana kwa miezi miwili mfululizo.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, hali hiyo imetokana na Serikali kushindwa kupeleka fedha za bajeti ya dawa MSD kwa wakati.

Pamoja na hali hiyo dawa ambazo zimekuwa  zikitumika sana Ciprofloxacin, Cetriaxone, Panadol, Diclofenac, Trimoxazol, Amoxycline, Doxycline na Metronidazol ambazo upatikanaji wake umekuwa wa kusuasua.

Taarifa iliyotolewa na MSD katika tofauti yake na uchunguzi uliofanywa zinaeleza kuwa kwa kupindi cha miezi mitatu mfululizo, kumekuwa na mtikisiko huo unaohatarisha afya za Watanzania kutokana na kukosekana dawa muhimu ikiwemo za maumivu.

Ingawa, serikali imeongeza fedha kwa ajili ya dawa muhimu na vifaa tiba kwa kiwango kikubwa kufikia Sh bilioni 250 kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 ikilinganishwa na Sh bilioni 29.2 zilizotengwa mwaka wa fedha uliopita 2015/16.

Kutokana na hali hiyo Serikali ilipaswa kuipa MSD Sh bilioni 62.5 katika kipindi cha Julai hadi Septemba lakini imepatiwa Sh bilioni 20 tu ambapo ni sawa na asilimia 32 pekee katika kipindi hicho.

Kilio sekta ya Elimu

Kwa upande wa sekta ya elimu, utafiti huo wa REPOA ulifanywa kwa walimu wa darasa la nne ambapo asilimia 60 ya walimu hao walibainika kuwa hawana ujuzi wa kufundisha.

Ingawa wastani wa ufaulu kwa somo la Kingereza na Hisabati kwa walimu ulikuwa ni wastani wa asilimia 59, lakini ni asilimia 21 tu walipata ufaulu wa wastani wa asilimia 80.

Dk. Katera,  alisema kutokana na hali hiyo, ufaulu wa wanafunzi katika masomo hayo ni wa chini.

Kuhusu upatikanaji wa rasilimali na miundombinu, utafiti huo umeonesha kuwa asilimia 69 ya shule hazina mahitaji ya msingi ambapo asilimia 53 ya shule hazikuwa na vyoo huku kwa upande wa upaikanaji wa vitabu ni mwanafunzi mmoja kati ya wane ndiye aliyekuwa na kitabu cha Hesabu au Kingereza.

Aidha mtafiti huo alibainisha kuwa licha ya walimu wengi kuhudhuria shuleni lakini hawaingii darasani kufundisha ambapo asilimia 47 hawakuwa darasani wakati wa vipindi vyao.

“Utafiti umeonyesha kwamba walimu wanatumia asilimia 12 ya muda wa kufundisha kwa siku kufanya mambo mengine hivyo wanafunzi kutumia saa 2:47 badala ya saa tano zinazotakiwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles