Mohammed Kassara -Dar es salaam
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa kikosi chake kimeiva kiasi kwamba anaumiza akili kupata kikosi cha kwanza kikali kitakachowamaliza mapema wapinzani wao, Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa kwanza ambapo timu hizo zitarudiana kati ya Agosti 23 na 25, mwaka huu, mjini Gaborone, Botswana.
Kuelekea mchezo huo, Yanga imejichimbia Visiwani Zanzibar na kucheza michezo miwili ya kirafiki na timu za Mlandege na Malindi FC kuhakikisha anakiweka sawa kikosi hicho tayari kwa mikikimikiki ya kimataifa na hata Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga ilianza kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mlandege, kabla ya kupepetena na Malindi FC katika mchezo wa pili wa kirafiki jana usiku.
Michezo hiyo ni mahususi kwa ajili ya Zahera kupata kikosi chake cha kwanza kutokana na kuchelewa kujiunga na timu hiyo wakati ilipoweka kambi mjini Morogoro kujiandaa na msimu mpya.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Zahera alisema kuwa licha wachezaji wake kucheza vizuri na kufunga mabao mengi kwenye michezo hiyo, viwango wanavyoonesha vinampa wakati mgumu kupata kikosi cha kwanza kitakachomaliza shughuli mapema dhidi ya Rollers.
Alisema kinachompasua kichwa ni kitendo cha kila mshambuliaji kufanya vizuri, hivyo bado anaumiza kichwa kupanga nani acheze na nani katika mchezo wa kesho.
“Kikosi kinaendelea kufanya vizuri, kila mchezaji hapa anajituma sana na kutoa alichonacho kwa ajili ya timu, wanafanya vizuri kila mmoja, hiyo inanipa kazi ya ziada kupata kikosi cha kwanza katika mchezo huo,” alisema.
Zahera alisema Juma Balinya na Patrick Sibomana wamekuwa wakifanya vizuri na kuelewana sana, kama ilivyo kwa Maybin Kalengo, Sadney Urikhob.
“Lakini hadi tunarudi Dar es Salaam kesho (leo), nitakuwa tayari nimejua nani anapaswa kuanza na nani, tunafahamu tunakutana na timu ngumu sana, tumepanga kuhakikisha tunamaliza mechi hiyo mapema hapa hapa nyumbani kabla ya kwenda ugenini,” alisema Zahera.
Akizungumzia kuhusu wachezaji wake watatu, Juma Abdul, Kelvin Yondani na Andrew Vicent ‘Dande’ ambao hawapo na kikosi hicho kwa muda mrefu, Zahera alisema ana taarifa za mmoja wao, lakini wengine akiwaachia viongozi wa Yanga.
“Kuhusu Yondani, aliniomba ruhusa nikamrusu, lakini Abdul na Dante, sina tatizo nao na matatizo yao yatamalizwa na uongozi wa juu, hivyo kila kitu kitakuwa sawa,” alisema.