33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Zahera afunguka mambo matano Yanga

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amefunguka mambo matano kuhusiana na klabu hiyo tangu msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara uanze.

Zahera mwenye uraia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Ufaransa, aliajiriwa na Yanga ili kurithi mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mzambia George Lwandamina, aliyeachana na timu hiyo Machi mwaka jana.

Tangu aanze kuifundisha Yanga msimu huu, Zahera, ameiwesha kushinda michezo 16 na kutoka sare miwili, baada ya kushuka dimbani mara 18.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kukusanya pointi 50 na kukamata uongozi wa Ligi Kuu, ikiwaacha washindani wake wa karibu Azam katika nafasi ya pili na pointi zao 40 na Simba kwenye nafasi ya tatu na pointi 33.

Ligi Kuu na ubingwa

Kocha Zahera akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema awali wakati ligi inaanza hawakuwa na fikra za kushindania ubingwa wa msimu huu, lakini kutokana na matokeo wanayopata hadi sasa wamekubaliana kuendelea kupambana kwa nguvu ili kubeba taji hilo.

“Tulianza maandalizi ya ligi zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya msimu kuanza, tulienda Morogoro huku timu nyingine zikiwa zimeanza maandalizi muda mrefu, ilitakiwa tufanye kwa wiki tano ila programu ya siku zote hizo tulifanya kwa wiki mbili.

“Tulianza ligi tukiwa hatuna malengo yoyote kutokana hali halisi iliyokuwa kwenye klabu, lakini hadi sasa tunaongoza ligi na tukiwa tumesaliwa na mchezo mmoja mkononi kabla ya mzunguko wa kwanza kuisha, hata kama ikitokea tumefungwa au tumeshinda bado tutakuwa tunaongoza ligi,” alisema.

“Nilikaa na wachezaji na kuzungumza nao kuhusu changamoto zinazowakabili na kuzifanya kuwa furaha, hatua hiyo iliwafanya wabadilike na kuwa na morali ya juu katika kila mchezo na kuifanya timu ipate matokeo.”

MICHUANO YA MAPINDUZI

Kuhusu michuano ya Mapinduzi alisema anafahamu umuhimu wa michuano hiyo, lakini hana kikosi kipana kitakachoweza kucheza michuano yote, ikiwamo ya Sport Pesa na Kombe la Shirikisho la Azam, huku wakiwa wanakabiliwa na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema kwa kulitambua hilo anatarajia kuwatumia wachezaji wake kulingana na programu zake.

“Kwa sasa kikosi changu kina wachezaji 20, kati ya hao saba ndio nawatagemea katika kuleta mabadiliko, wengine ni majeruhi kama Andrew Vincent ‘Dante’,  Juma Mahadhi, Raphael Daud, Baruan Akilimali, Papy Tshishimbi yuko DRC kutokana na matatizo ya kifamilia, hivyo nitawachezesha wachezaji kulingana na programu yangu.

“Huwezi ukawa unakimbiza sungura watatu kwa wakati mmoja na ukawashika, itafika wakati itakubidi umkimbize mmoja ili uweze kumshika,  tutaenda kwenye michuano ya Mapinduzi lakini tutacheza kulingana na programu yetu,” alisema.

MASHABIKI YANGA

Zahera alisema kati ya nchi tisa za Afrika alizowahi kuzitembelea hakuna hata moja yenye mashabiki wengi wa soka kama ilivyokuwa kwa Tanzania.

“Nimeshangazwa sana na wingi wa mashabiki wa hapa Tanzania hasa kwa timu hizi mbili Simba na Yanga, kwani nimetembea takribani nchi tisa Afrika, lakini sijakutana na sehemu yenye mashabiki wengi, hata timu kama TP Mazembe haina mashabiki wengi namna hii.

“Unakuta tunaenda kucheza mikoani lakini idadi ya mashabiki inaendelea kuwa vile vile, hali hiyo inatutia sana nguvu sisi pamoja na wachezaji ambao wanacheza kwa kujitoa na kupata matokeo,” alisema.

UGOMVI WAKE NA KAKOLANYA

Baada ya kuweka wazi msimamo wake wa kutokuwa tayari kufanya kazi na kipa wake, Beno Kakolanya, kutokana na kile alichodaiwa ni mtovu wa nidhamu, Zahera alisema lolote linaweza kutokea kwa sasa.

“Suala la Kakolanya bado lipo, mnaweza mkamwona akiendelea kucheza au la, lakini kwa sasa bado nafikiria,” alisema.

 UONGOZI YANGA

Kocha huyo amesisitiza kuwa hana mgogoro wowote na mabosi wake Yanga tofauti na baadhi ya watu wanavyodhani.

“Mimi huwa napenda kuongea ukweli, hii haimaanishi ukisema ukweli ndio umegombana na mtu, hapana. Naongea na kila kitu kinaisha hapo hapo,” alisema.

Zahera alitoa matamshi hayo akirejea hatua yake ya kuulaumu wazi wazi  uongozi wa klabu yake kwamba ulimdanganya kuhusu mapendekezo yake ya kutaka wasajili wachezaji watatu wakati wa usajili wa dirisha dogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles