Na VICTORIA GODFREY-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAA), umesema upo tayari kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Katibu Mkuu wa ZAA, Yassin Muhidini alisemaushiriki wao ni katika riadha ya mbio fupi.
Alisema kuwa, mpango wa ZAA ni kuhakikisha inapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kusaka viwango vya kufuzu michezo ya Olimpiki ijayo.
“Malengo yetu tunataka kuhakikisha kila mashindano ya kusaka viwango yatakavyotakangazwa katika nchi mbalimbali, tutakuwa tunapeleka ili washiriki kikamilifu na kupata nafasi ya kushiriki michezo ya Olimpiki.
“Zanzibar tunajivunia sana kuwa na wanariadha wazuri wanaoshiriki mbio fupi kutokana na asili ya mbio hizi ni huku, hivyo tunayo mipango ambayo tunatumia fursa ya kipindi hiki cha janga la corona ili tuweze kutimiza malengo yetu,”alisema Muhidini.
Alisema ili kufikia malengo hayo, wanariadha wenyewe wanatakiwa kujituma kwa bidii kufanya mazoezi yao binafsi kwa kufuata program za mazoezi wanazopewa na makocha wao .