23.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

YUDA THADEY: MLEMAVU MWENYE VIPAJI LUKUKI ANAYEWIKA MWANGA

Yuda Thadey akiwa kazini

Na Mwandishi Wetu,

UNAPOKUTANA ana kwa ana na kijana Yuda Thadey, lazima nafsi yako itaurejea utukufu wa Mungu. Hakika hutoamini kwamba kijana huyo mlemavu aliyepooza kuanzia kiunoni hadi miguuni anafanya kazi nzito za ufundi ambazo si rahisi kufanywa na mtu wa kawaida tena mwenye elimu ya kawaida kama yeye.

Kijana huyo anapatikana katika Wilaya ya Mwanga, Ugweno mkoani Kilimanjaro. Jina lake ni maarufu wilayani humo kutokana na kipaji alicho nacho.

Akizungumza na gazeti hili, Thadey anasema kuna wakati anafanya kazi bila kulala. Wakati mwingine hutumia zaidi ya saa 20 kufanya kazi.

Anasema anapoanza jambo lake hataki liishie njiani hivyo uhakikisha anamaliza ndipo huendelea na kitu kingine.

Kijana huyo ni mahiri katika kutengeneza vifaa vyote vya umeme ikiwamo simu, kompyuta, redio na runinga. Pia anao uwezo wa kuhariri video na kurekodi, mtayarishaji wa muziki wa aina yoyote licha ya kwamba amebobea katika muziki wa Injili ambao anaupenda kwa sababu ameokoka.

Anasema aligundua kipaji chake baada ya kuanza kutengeneza saa na baadae redio, ambapo kila siku alikuwa akichukua betri za redio na kugombezwa na mama yake.

Anasema aliongezewa ujuzi wa vitu mbalimbali kutoka kwa jirani yao aliyejulikana kwa jina la Mzee Juma.

“Nikiwa na Mzee Juma nilikuwa nikijifunza jinsi ya kutengeneza redio, lakini yeye alikuwa akitumia vifaa ambavyo si halisi hivyo, kwa sababu napenda kusoma nilisoma na kuvijua vile vya kitaalamu,” anasema.

Anasema sasa hivi anajifunza masuala ya mtandao, hivyo huamka saa 12 asubuhi na kuamsha watoto kwa ajili ya kwenda shule baada ya hapo anaanza kutengeneza runinga au redio hadi saa 12 jioni, kisha anawasha kompyuta na kuanza kujifunza mambo mbalimbali ya intaneti.

Akizungumzia fani anayoipenda anasema utangazaji ndio ilikuwa ndoto yake kuu na kwamba huenda ndiyo chanzo cha yeye kupenda ufundi wa redio na TV.

Licha ya kutengeneza vifaa vya umeme, Thadey pia ni mwalimu wa muziki wa aina zote ambapo anatunga na kuimba, anapiga kinanda, gitaa na kurekodi japo kwa sasa anashindwa kwa sababu ana maumivu ya kifua.

Anasema maumivu hayo yanatokana na kazi ya kufungua redio na televisheni.

Yuda Thadey akiwa na baba yake, George Kajiru

Hata hivyo, Thadey anasema anapotengeneza kompyuta, saa na vitu vingine huwa havimdhulu.

Hivi majuzi alifanya kazi ya kuwarekodi wanakwaya wa kwaya ya Mtakatifu Theresia Kikweni Ugweno, ambao aliwatengenezea kuanzia ala na video huku akirekodi video hiyo kwa kutumia simu yake ndogo ya mkononi jambo lililowashangaza wengi.

Kazi hiyo aliifanya katika mazingira magumu kwani walikosa hata chumba maalumu cha kuchukulia sauti pia hawakuwa na vipaza sauti hivyo alitumia akili ya ziada kwa kutengeneza mfumo ambao aliweza kuchukua sauti za wanakwaya wote kwa pamoja. Thadey anasema kurekodi bongo fleva ni rahisi zaidi kuliko kwaya.

Thadey amekuwa ni mtu muhimu kwa wakazi wa Wilaya ya Mwanga kwani amekuwa akitoa elimu na ujuzi walionao kuwafunza vijana ili nao waweze kujiari kwa kutumia vipaji vyao.

Thadey anasema alishawahi kutengeneza masafa ya Fm bila kujua na kuanza kupiga miziki yake.

Anasema kuwa suala hilo lilitaka kumletea matatizo baada ya kuingiliana na masafa ya redio mojawapo nchini ambayo ilianza kukoroma na kutosikika vizuri.

“Wahusika walinifuata kutaka kunikamata lakini walipoiona hali yangu wakanihurumia na kunielimisha kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria,” anasema.

Anasema pia aliwahi kutengeneza simu ya mkononi kwa kutumia vifaa vyake na ikawa inafanya kazi vizuri.

Anasema baada ya kuitengeneza aliijaribu kwa kuwapa vijana na kwenda umbali tofauti kasha kuwapigia simu ikawa inafanya kazi vizuri.

Akatisha masomo

Alizaliwa Novemba 9, 1973 akiwa mzima hana tatizo lolote. Alipokuwa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kisanjuni, alianguka kutoka juu ya mti wa mzambarau, wakati akijaribu kuchuma zambarau.

Hii ilikuwa mwaka 1985, baada ya kuanguka alipelekwa katika Hospitali ya Kifura mkoani Kilimanjaro.

Kutokana na hali yake kuwa mbaya alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi na kulazwa kwa muda wa miezi mitano, baada ya madaktari kubaini kuwa amevunjika uti wa mgongo. Baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya KCMC, lakini kutokana uhaba wa fedha alirudishwa Mawenzi.

Aliporudi nyumbani kwao Ugweno, madaktari walimshauri awe anahudhuria mazoezi katika Hospitali ya Mawenzi lakini alishindwa kutokana na kuvunjika mguu akiwa mazoezini.

Thadey anasema; “nilishindwa kwenda hospitali baada ya kuvunjika mguu nikiwa nyumbani nafanya mazoezi kitandani,” anasema.

Anasema baada ya hapo akapelekwa katika Hospitali ya Kifura na kulazwa kwa miezi minne.

“Niliporuhusiwa kurudi nyumbani, baada ya mwaka mmoja nilivunjika tena mguu wa pili wakati naamka kitandani,” anasema.

Thadey anasema kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa yeye kuendelea na shule licha ya kwamba alikuwa akiongoza darasani kwa kuwa mwanafunzi wa kwanza kuanzia darasa la kwanza hadi la tatu.

Akiwa nyumbani baba yake aliamua kuendelea kumfundisha kusoma vitabu na magazeti jambo ambalo lilimsaidia kuwa mjuzi wa mambo mbalimbali.

 Matatizo yamuandama

Historia ya Thadey imejaa mikasa kwani hadi kufikia kuwa fundi anayetegemewa na wilaya nzima, aliwahi kumsababishia baba yake kufungwa mwaka mmoja katika gereza la Kilulu kwa kosa la kukutwa na nyaya za simu lakini mwenyewe anasema zilitegeshwa.

Akizungumzia mkasa huo, baba mzazi wa Thadey, George Kajiru anasema kuna kijana ambaye aliiba redio kwa dada mmoja ambaye ni mwalimu aliyejulikana kwa jina moja la Rose na kumuuzia mwanawe kama spea na kwamba hakukuwa na kitu kingine zaidi ya hiyo.

Baadaye Rose alibaini kuwa redio yake ipo kwa Thadey hivyo alitaka suala hilo liende polisi, ambao walipofika kumkagua wakaziona nyaya za simu, ikabidi waondoke na Kajiru.

Anasema alipofika polisi alifunguliwa jarada na kesi ikapelekwa mahakamani ambako alikutwa na hatia akahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela katika gereza la Kilulu.

“Nilipomaliza kifungo baadaye ikabainika kuwa zile nyaya zilikuwa zimefichwa na mtu mwingine lakini kwa sababu tayari nilishatoka jela haikuwa na maana tena. 

Afya mgogoro

Thadey anasema kuwa licha ya kufanya kazi hizo, afya yake ni mgogoro kutokana na mazingira anayofanyia kazi, pia kazi anayoifanya ya kutengeneza vifaa vya umeme.

Anasema kazi hiyo imemfanya aumwe kifua mara kwa mara kutokana na kuifanya huku akiwa amelala.

Pia anasema kuwa huwa anasumbuliwa na ugonjwa wa UTI. “Hali hii inasababishwa na mpira ambao nimefungwa kwa ajili ya kujisaidia, hivyo dumu linalopokea haja ndogo likijaa na kukosekana mtu wa kuumwaga huwa unarudi katika mpira na hivyo kuniletea madhara,” anasema.

 Changamoto za kikazi

Thadey anasema kuwa kumekuwapo watu ambao huwakusanya walemavu na kuwaambia kuwa wanataka kuwapatia mikopo lakini haiwasaidii kutokana kwamba wanapewa kwenye makundi na hivyo inapotokea mmoja wao ameshindwa kulipa hujikuta wakiingia gharama zaidi.

Anashauri taasisi za mikopo kuwafikia na kuzungumza nao kila mmoja kwa wakati wake na si kwa vikundi ili kujua hitaji la mtu na kuwakopesha mmoja mmoja ili kila mhusika abebe msalaba wake.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni kukatika kwa umeme na ulipaji wa bili kubwa huwa unamuumiza.

Anasema ameshaomba mara kadhaa abadilishiwe mita na kupewa ya Luku bila mafanikio.

Anasema anachokiwaza sasa ni kununua umeme wa jua kuwa kuwa utamrahisishia kufanya kazi bila kulipa gharama kubwa za umeme.

 Ushauri

Anawashauri mafunzi wenzie wapende kusoma ili kujua mambo mengi zaidi. 

Ombi kwa Rais

“Naomba Rais Dk. John Magufuli anisaidie nipate umeme wa jua hapa studio ili nifanye kazi zangu kwa ufasaha bila kuogopa gharama za umeme,” anasema na kuongeza:

“Rais anataka Tanzania ya viwanda, ili atomize adhma yake  aanze na sisi vijana wenye ujuzi lakini hatuwezi kuuendeleza kwa kukosa fedha.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,293FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles