31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yondani aipaisha Yanga

Pg 32*Yachomoza kwa Ndanda na kuishusha Azam kileleni

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Yanga jana iliendeleza kasi yake kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa Ndanda FC ya Mtwara bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kuishusha  Azam FC kileleni mwa ligi hiyo.

Matokeo ya jana yameiwezesha Yanga kurejea kileleni kwa kufikisha pointi 36 sawa na Azam wanaoshika nafasi ya pili wakitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Vinara hao tayari wamepachika wavuni jumla ya mabao 31 huku wakikubali nyavu zao kutikiswa mara tano, ikiwa ni tofauti ya mabao matatu ya kufunga dhidi ya wapinzani wao Azam waliofunga mabao 28 na kufungwa mabao tisa.

Yanga na Azam zimekuwa zikipeana zamu ya kuongoza katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 16, hivyo kama Azam watashinda keshokutwa dhidi ya Mgambo Shooting watafanikiwa kurejea kileleni.

Katika mchezo wa jana, timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu ndani ya dakika 15 za awali ambapo wenyeji Yanga walikuwa wakimtumia winga, Deus Kaseke kupandisha mashambulizi langoni kwa Ndanda.

Dakika ya 29 beki Juma Abdul nusura aipatie Yanga bao la kuongoza akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga lakini shuti alilopiga akiwa nje ya eneo la hatari lilipanguliwa na kipa wa Ndanda, Jeremia Kisubi.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Yanga walikosa penalti dakika ya 48 iliyopigwa na mshambuliaji wa kimataifa, Amissi Tambwe na kugonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani.

Hata hivyo, mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza, aliamuru penalti hiyo ipigwe kuelekea lango la Ndanda baada ya kiungo Simon Msuva wa Yanga kufanyiwa madhambi na Paul Ngalema.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 59 Yanga walifanikiwa kupata penalti nyingine  iliyofungwa na Kelvin Yondani, baada ya Kaseke kufanyiwa madhambi na mchezaji wa Ndanda akiwa katika harakati ya kuokoa mpira.

Baada ya kupata bao la kuongoza, Yanga walifanya mabadiliko ya kuwatoa Kaseke na Tambwe na nafasi zao kuchukuliwa na Issoufour Abubacar na Malimi Busungu, huku Ndanda wakimtoa Kigi Makasi na kumwingiza Masoud Ally.

Mabadiliko hayo yaliisaidia zaidi Ndanda ambao muda mwingi walionekana kuwa imara na kuwafanya wapinzani wao kuongeza umakini wa kulinda bao lao licha ya kufika mara kwa mara kwenye lango lao.

Yanga: Deogratius Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vicent Bossou, Kelvin Yondani, Salum Telela, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Malimi Busungu na Deus Kaseke/Issoufour Abubacar.

Ndanda: Jeremia Kisubi, Azizi Sibo, Paul Ngalema, Kassian Ponera, Salvatory Ntebe, Jackson Nkwera, William Lucian, Hemed Khoja, Atupele Green, Kiggi Makasi na Braison Raphael.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles