Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WAZIRI wa zamani wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba, Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja wamefunga utetezi na sasa wanasubiri hukumu ya mahakama.
Washtakiwa hao kupitia mawakili wao, Elisa Msuya na Beatus Malimi waliiarifu mahakama hiyo jana mbele ya Jopo la mahakimu watatu linaloongozwa na Jaji John Utamwa, kwamba kwa ushahidi uliotolewa hawaoni haja ya kuita shahidi mwingine.
Jopo hilo ni Majaji John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela.
“Tulitegemea kupata shahidi wa pili kwa ajili ya washtakiwa lakini baada ya kuangalia ushahidi uliotolewa tumeona hatuhitaji shahidi mwingine,”alidai.
Washtakiwa wote wanakabiliwa na kesi ya kutumia madaraka vibaya na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Wakili Msuya baada ya kufunga ushahidi huo kwa wateja wake mshtakiwa wa kwanza na wa pili, aliomba kuwasilisha hoja za mwisho kabla ya kutolewa hukumu.
Wakili Malimi alidai kwa upande wa mshtakiwa wa tatu (Mgonja), pia wanaomba kufunga kesi yao. Baada ya kuomba kufanya hivyo, Jaji Utamwa alisema kesi ya upande wa utetezi imefungwa.
Upande wa utetezi uliomba kuwasilisha majumuisho yao ya mwisho, ambao walitakiwa kuwasilisha kwa pamoja kwa washtakiwa wote.
Wakili Msuya aliomba mahakama iwapatie mwenendo wa kesi kwa upande wa utetezi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro pia aliomba kupatiwa mwenendo huo kwa ajili ya kuandaa majibu ya majumuisho ya mwisho.