27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga yaua Zanzibar

ngoma na mafunzo*Yaitungua Mafunzo 3-0, Kamusoko, Ngoma tishio

NA MWANDISHI WETU

TIMU ya soka ya Yanga jana ilianza kwa kishindo michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuishushia kipigo cha mabao 3-0 timu ya Mafunzo katika mchezo wa ufunguzi uliopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kipigo cha Yanga kwa Mafunzo ni salamu tosha kwa wapinzani wao, Azam FC ambao wamepangwa kundi B kwenye michuano hiyo ambayo inahusisha jumla ya timu nane kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na URA kutoka Uganda.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, walicheza kwa kujiamini zaidi na kuonyesha wamepania kuwavua ubingwa watani wao wa jadi, Simba tofauti na mwaka jana ambapo walitolewa hatua ya robo fainali na JKU ya Zanzibar.

Yanga walioingia uwanjani wakiwa na morali ya kuibuka na ushindi, walifanya shambulizi kali langoni kwa Mafunzo  dakika ya 12 kupitia kwa mshambuliaji wake, Amissi Tambwe, aliyeunganisha vyema pasi ya Simon Msuva lakini haikuzaa matunda.

Dakika ya 27, Tambwe alikosa bao la wazi baada ya kupiga shuti hafifu la mpira wa adhabu lililotokana na Donald Ngoma kufanyiwa madhambi ambalo lilitoka nje ya lango.

Yanga walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 31 kupitia kwa Ngoma aliyepiga shuti kali akiunganisha pasi safi ya Thabani Kamusoko ambaye kasi yake imeanza kuwavutia wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.

Wakati Mafunzo wakitafuta mbinu za kusawazisha bao hilo, walijikuta nyavu zao zikitikiswa kwa mara nyingine ambapo dakika ya 34, Ngoma aliipatia timu yake bao la pili akiunganisha pasi ya Kamusoko.

Baada ya kupokea mashambulizi mengi kutoka kwa Yanga, Mafunzo walizinduka na kupata faulo dakika ya 66 nje kidogo ya eneo la hatari lakini walishindwa kutumia nafasi hiyo kwa kupiga shuti hafifu lililotoka nje ya lango.

Dakika ya 70, Yanga walifanya mabadiliko ya kuwatoa Kamusoko, Godfrey Mwashiuya na nafasi zao kuchukuliwa na Sina Jerome na Deus Kaseke huku Mafunzo wakimtoa Jermane Said na kumwingiza Jerome Hassan.

Dakika ya 80, Mafunzo walipata penalti baada ya Shaban Suleiman kufanyiwa madhambi na beki, Kelvin Yondani, lakini kipa wa Yanga, Deogratius Munishi aliweza kupangua mkwaju huo uliopigwa na Aboula Azizi.

Mshambuliaji Paul Nonga aliyeingia kipindi cha pili kuiongezea kasi Yanga, alifanikiwa kuiandikia bao la tatu timu yake dakika ya 89 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Mafunzo na kupiga shuti lililojaa wavuni.

Mchezo mwingine wa Kundi B kwenye michuano hiyo ulitarajiwa kuchezwa jana usiku kwa kuzikutanisha timu za Azam na Mtibwa Sugar.

 

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles