Na Daines Msumeno,TUDARCo
Kikosi cha Yanga kimewasili mjini Bukoba leo Septemba 27, kwa maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Jumatano Septemba 29, 2021 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Yanga imetua kifua mbele ikiwa imetoka kubeba ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Simba bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Jumamosi iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Yanga, Haji Manara amesema timu imeondoka na wachezaji 25 na benchi zima la ufundi na wamewasili salama, huku wakipata mapokezi makubwa.
“Leo mnafahamu timu imeondoka kuelekea Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. wameondoka kamili na wachezaji 25, tunakwenda kukutana na Kagera Sugar ni timu nzuri.
“Tunajua wana kikosi imara umeona usajiri wao na wana walimu ‘very smart’. Kwa hiyo tunafahamu mechi ngumu. Tumefurahi mapokezi waliyopata wachezaji wetu wachukulie yale mapokezi kama deni kwa mashabiki,” amesema.
Katika hatua nyingine Manara ametamba kuwa sherehe za raha ya kuwafunga watani wao wa jadi Simba na kutwaa taji la Ngao ya Jamii, zimekwisha na jukumu lililobaki ni kuusaka ubingwa Ligi Kuu.
“Sherehe zimeisha kwa sasa hatuhitaji sherehe, tumesheherekea juzi usiku kucha,jana sasa tunakwenda kuanza ligi kuu. Wote tunajua Wanayanga, miaka minne mfululizo hatujashinda taji hili la ubingwa Ligi Kuu.
“Kiu ya Wanayanga haikuwa jambo lolote isipokuwa kushinda Ngao ya Jamii, ubingwa wa ligi kuu, ubingwa wa FA na Mapinduzi Cup, ndio mataji tulobaki nayo matatu. Moja tumelishinda juzi.
Aidha amewataka mashabiki kuacha kulalamika bali kuelekeza nguvu katika kusapoti timu na kuwekeza kupata matokeo mazuri.