Lulu Ringo, Dar es Salaam
Klabu ya Yanga imeunda kamati mpya ya uchaguzi mdogo ambayo itashirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), katika uchaguzi kwa nafasi za viongozi zilizoachwa wazi baada ya wengine kujiuzulu.
Viongozi waliojiuzulu nafasi zao katika klabu hiyo ni Mwenyekiti Yusuph Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, wajumbe Hashimu Adballah, Salum Nkemi, Omary Said na Ayoub Nyenzi.
Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 13 mwaka huu, lakini ulihairishwa baada ya baadhi ya wanachama kwenda kuweka pingamizi mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya klabu hiyo, leo Februari 21, Makamu mwenyekiti wa Yanga, Siza Lyimo, amesema tayari uongozi umeshachagua kamati ya uchaguzi ambao itaongozwa na Venance Mwamoto Mbunge wa Kilolo Iringa, na katibu wake Seif Gulamali Mbunge wa Igunga, Dastan Kitandula Mbunge wa Mkinga na Saidi Mtanda Mkuu wa Wilaya na Nkasi.
“Yanga kwa kushirikiana na TFF tayari tumepata majina manne mengine ya kamati ya uchaguzi, kwa kuwa mwanzo tulipeleka majina lakini yalipoteza sifa hivyo tukaunda kamati nyingine, naamini uchaguzi huo kwa kushirikiana na wanayanga utakwenda vizuri,” amesema Siza
Aidha Mkuu wa Kitengo cha Habari wa klabu hiyo, Dismas Ten, amesema timu ya Yanga inatarajia kuondoka kesho kwenda Mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Namungo FC katika hatua ya 16 Bora, mchezo utakaochezwa Jumapili Februari 24, Uwanja wa Majaliwa mkoani wa humo.
Dismas amesema ratiba bado ya michezo mbalimbali ya klabu yao bado haijakaa vizuri ukizingatia na umbali wa sehemu wanazoenda kucheza kwa kuwa hali hiyo imekuwa changamoto kubwa katika timu.
“Tumetoka kucheza Mwanza, tumerudi tunaenda kucheza na Namungo FC , baada ya hapo tutaenda tena Mwanza kucheza dhidi ya Allience na timu itarudi tena Dar es Salaam kucheza na KMC na baada ya hapo itelekea tena Iringa kucheza na Lipuli FC, hivyo hali hii inaweza kuleta changamoto ya timu kutofanya vizuri hivyo tunaomba bodi ya ligi kutazama kwa umakini suala hili,” amesema Dismas.
Katika hatua nyingine Mtaribu wa klabu hiyo, Hafidhi Salehe, ametaja kiasi cha fedha ambacho kimepatikana hadi kufikia leo Februari 21 tangu kuanzishwa kwa mchakato wa kuchangia timu hiyo na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera mwanzoni mwa Februari mwaka huu katika miamala ya M Pesa, Tigo Pesa na Benki ya CRDB.
“Wakati tunaanza mchakato huu tuliwaahidi wadau kuwa tutakuwa tunatoa mrejesho kila wiki lakini kutokana na ratiba kubana hatukuweza kufanya hivyo, mpaka sasa tumekusanya zaidi ya Sh milioni 21 kutoka kwenye Tigo Pesa, M pesa na akaunti ya benki ya CRDB.
“ Tunashukuru kwa wadau ambao wameendelea kutuchangia lakini bado kiasi hiki cha fedha hakitoshi kutokana na mahitaji ambayo kocha alisema anahitaji kuyatimiza hivyo tunaomba muendelee kujitolea kuisaidia timu,” ame sema.