Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
BENCHI la ufundi la Yanga limeshtuka kwamba mbinu yake ya kusaka mabao kupitia katikati, imekuwa ikiwapa wakati mgumu pale wanapokutana na safu makini ya ulinzi na kuamua kurejea pembeni kama ilivyokuwa ikifanya msimu uliopita.
Yanga ilibadili mbinu yake ya kusaka mabao kupitia pembeni, baada ya kumuuza katika klabu ya Difaa Al Jadida ya Morrocco aliyekuwa winga wa timu hiyo, Simon Msuva anayesifika kwa kasi.
Benchi la ufundi la Yanga chini ya Kocha George Lwandamina lilimpa Msuva majukumu ya aina mbili; moja likiwa kupiga krosi akitokea upande wa kulia na jingine kufunga na yote alikuwa aliyatekeleza kwa ukamilifu mkubwa, huku upande wa kushoto likimpa kazi ya kupiga krosi beki Haji Mwinyi.
Krosi hizo zilikuwa zikitumiwa vema na washambuliaji wa timu hiyo, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Donald Ngoma ambao kila mmoja alikuwa moto katika kupachika mabao yaliyoiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania kwa mara ya tatu mfululizo pamoja na kufunga jumla ya mabao 57, hivyo kuwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi.
Lakini baada ya Msuva kuondoka na ujio wa wachezaji wapya katika kikosi cha timu hiyo, benchi la ufundi la Yanga liliamua kubadili mbinu kwa kuanza kusaka mabao kupitia katikati na jukumu hilo wakipewa viungo, Thaban Kamusoko na Papy Kapamba Tshishimbi.
Yanga ilionekana ikitumia mbinu hiyo katika mechi za maandalizi ya msimu mpya, mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na ule wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati yake na Lipuli.
Licha ya kucheza vizuri katika mchezo dhidi ya Simba, safu ya ushambuliaji ya Yanga ilionekana kukosa mbinu za kupenya katikati na kufunga mabao, hatua iliyosababisha kupoteza mchezo kwa kulala kwa penalti 5-4. Hali hiyo ilijirudia kwenye mchezo dhidi ya Lipuli ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli.
Katika mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alionekana akiwapanga mabeki, Ramadhani Kessy na Juma Abdul upande wa kulia, huku kushoto akiwatupa Haji Mwinyi na Thabani Kamusoko na kuwapa kazi ya kupiga krosi kisha wachezaji wengine kutakiwa kufunga.
Baada ya zoezi hilo kukamilika, Nsajigwa aliwapanga kwa kugawa makundi mawili ya wachezaji; la kwanza likiwa na Juma Mahadhi, Pius Buswita, Canavarro, Maka Edward, Said Juma, Kessy, Matheo Antony, Pato Ngonyani na Mwinyi.
Jingine lilikuwa na Abdul, Andrew Vincenti ‘Dante’, Ninja, Juma Makapu, Kabamba Tshishimbi, Yusuph Mhilu, Donald Ngoma na Ibrahim Ajib ambapo ilipigwa mechi ya maana.